Enock asimulia alivyosota gerezani miaka 10 bila hatia

Enock asimulia alivyosota gerezani miaka 10 bila hatia

Muktasari:

  • Hujafa hujaumbika, ndivyo unavyoweza kusema juu ya mkasa uliowakuta Enock George na wenzake watatu walipokamatwa na Polisi mwaka 2010 wakidaiwa kuhusika katika mauaji ya mtoto Jesca Jonathan maeneo ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Hujafa hujaumbika, ndivyo unavyoweza kusema juu ya mkasa uliowakuta Enock George na wenzake watatu walipokamatwa na Polisi mwaka 2010 wakidaiwa kuhusika katika mauaji ya mtoto Jesca Jonathan maeneo ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Enock na wenzake walikamatwa baada ya Jesca kukutwa amekufa kichakani akiwa na dalili za kuchomwa na vitu vyenye ncha kali, hivyo wao walishukiwa kwa kuwa walikuwa wakicheza naye mara kwa mara.

Gazeti la Mwananchi, lilimtafuta Enock, baada ya kesi yao kutajwa kwenye barua ya mwanaharakati Tito Magoti aliyemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan akitaka Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ipitiwe upya kwa kuwa inakandamiza haki za binadamu.

Kwa mujibu wa Magoti, watoto hao walishtakiwa kwa kosa la mauaji, lakini wamezungushwa kwa takribani miaka 10 bila kukutwa na hatia na kuachiwa kwa utaratibu wa Nolle Prosequi.

Akizungumza na Mwananchi juzi jijini Dar es Salaam, Enock amesema alikuwa na miaka 13 alipokamatwa na wenzake.

“Aliyefariki alikuwa dada yangu binamu, alikuwa ni mtoto wa mjomba na tulikuwa tukicheza naye mara kwa mara, ila siku alipokufa sikuwa naye.

Baada ya wazazi wake kwenda Polisi kutoa taarifa, tukaja kukamatwa kwa kuwa ni majirani. Tulikuwa wanne, japo mmoja wetu alitoroka,” amesema.

Alisema baada ya mahojiano na Polisi walipelekwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kisha wakapelekwa rumande gereza za Segerea.

Anasema tangu wakati huo kesi iliendelea katika mahakama hiyo, lakini baadaye ilionekana kuwa imekosewa. “Mheshimiwa hakimu (alimtaja jina) alisema kesi hiyo imekosewa, kwa hiyo akataka irudishwe tena kituo cha polisi iandikwe upya, wakati wameshapoteza miaka miwili gerezani.

“Tulirudishwa kule Kigamboni kituo cha Polisi baada ya kukaa miaka miwili gereza la Segerea, mashtaka yakaandaliwa upya, kesi ikapelekwa Mahakama ya Kisutu na tukahamishiwa jela ya watoto iliyopo Upanga,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa walikaa katika gereza hilo la watoto kwa miaka mitatu wakisubiri wapangiwe tarehe ya kesi.

“Baada ya miaka mitatu tukapelekwa mahakamani ambako tuliambiwa mashitaka yamekosewa tena, tukaachiliwa huru halafu tukakamatwa tena.

“Tukarudishwa tena kituo cha Polisi Kigamboni mashitaka yakaandikwa upya kisha tukarudishwa gereza la watoto Upanga, lakini kule wakatukataa wakisema tumeshakuwa wakubwa, hivyo tukarudishwa kituo cha Polisi Kigamboni.”

Baada ya kurudishwa kituo cha polisi, wanasema walirudishwa tena mahakama ya wilaya ya Temeke, ambako walipelekwa tena rumande gereza la Keko ambako walikaa miezi miwili.

“Wakati huo walisema tumeshakua, kwa hiyo wakawa wanatupeleka magereza ya watu wazima.

Lakini baada ya miezi miwili ya kuishi Keko, wakasema wamekosea kutuweka pale kwa sababu sisi bado ni watoto, wakatuhamishia tena gereza la Segerea,” anasimulia.

Ilipofika mwaka 2017 anasema ndipo kesi yao ikaanza kusikilizwa tena, lakini wakawa wakisubiri kuitwa mahakamani.

“Tulikaa pale miaka miwili tukisubiri wito wa mahakama na tulipoitwa mahakama ya Kisutu, Hakimu akasema kesi imekosewa tena, kwa hiyo inabidi turudi kituo cha Polisi ili ikaandikwe upya.

Lakini wakati huo kesi ilishaanza na mashahidi wameshatoa ushahidi wao,” ameeleza. Anaendelea kusema baada ya kauli ya hiyo ya hakimu, waendesha mashitaka walijadiliana na kuamua kukata rufaa. “Tulikaa tena zaidi ya mwaka mzima Segerea tukisubiri kupelekwa kwenye rufaa,” amesema.

Kuachiwa huru

Ameendelea kusimulia kuwa wakati wanaendelea kusubiri kupelekwa kwenye rufaa, Juni 2020 wakapelekwa Mahakama Kuu ambako shauri lao lilisikilizwa kwa muda mfupi, kisha wakaambiwa warudi baada ya siku tatu.

“Tuliporudi tukaambiwa mahakama imeamua kesi iendelee, lakini waendesha mashitaka waliamua wasiendelee na kesi, japo wakati huo walikuwa wamekata rufaa. Kwa hiyo tukaachiwa huru,” anasema.

Elimu

Enock anasema wakati anakamatwa alikuwa darasa la pili na tangu hapo hakupata haki ya kumaliza elimu ya msingi.

“Tulipopelekwa gereza la watoto Upanga niliendelea kusoma mpaka darasa la sita, kwa sababu pale kuna shule na kuna utaratibu wake.

Tunaamka asubuhi, tunajiandaa unavaa sare kisha tunapewa uji ndiyo tunaingia darasani.

 “Kila mfungwa anaulizwa darasa aliloishia na ndiyo anaendelea hapo hapo. Kuna ukumbi mmoja tu ambao wote tunachanganywa humo na mwalimu yupo mmoja ambaye anafundisha madarasa yote kuanzia shule ya msingi hadi sekondari,” anasema.

Ameeleza kuwa hata wakati wa kufanya mitihani ya kitaifa, hutolewa na kupelekwa kwenye shule walizotoka na kufanya mitihani hiyo na jioni hurudishwa gerezani.

Hata hivyo, anasema kutokana na kuhamishwa magereza, hawakuweza tena kuendelea na masomo hayo. “Nilipotoka gerezani sikuendelea na masomo.

Kwa sasa kazi zangu ni kusaidia mafundi ujenzi. Wenzangu wapo, mmoja amesafiri na mwingine yupo hapa Dar es Salaam amejiajiri ni dereva,” amesema.

Enock ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto watano. Wadogo zake bado wanaendelea na masomo. Hata hivyo, kwa sasa amepoteza matumaini ya kuendelea na shule.

“Kwa sasa kama itatokea fursa ya kurudi shule nitakwenda kwa sababu kama ni muda nimepoteza muda mwingi na haki yangu ya elimu kama mtoto.

Ila kwa sasa wazazi wangu hawana kipato cha kuniwezesha kurudi shule,” anasema.

Ameiomba Serikali iwaangalie watuhumiwa wengine hasa watoto wasipoteze muda mwingi magerezani. “Wapo watu waliokaa magerezani kwa muda mrefu bila kushitakiwa; kuna wengine nimewakuta nimewaacha, wengine wamenikuta nimewaacha.

“Ninachoiomba Serikali waangalie uwezekano wa kutoweka watu magereza muda mrefu bila hatia kama sisi tulivyofanyiwa,” amesema.

Hatasahau mateso ya jela

Kuhusu mateso ya gerezani, Enock anatofautisha magereza ya watoto na ya watu wazima akisema amepitia mateso mengi. “Kule kwa watoto mnakuwa na ratiba ya kusoma, kufanya usafi, kupika na kucheza. Ila tu hakuna uhuru zaidi ya hapo.

Lakini kwenye magereza ya watu wazima kuna mateso zaidi. Kule mazingira ya kuishi ni magumu. Sawa watu wanaishi, utakula utashiba, lakini siyo chakula kizuri,” anasema.

 Akieleza zaidi mateso waliyopata, Enock anasema amani hutoweka gerezani ukifika wakati wa ukaguzi maalumu. “Kuna askari wanaitwa KM wenye vibaka vya kijani. wale wakiingia gerezani kuna jambo maalumu na amani ya gereza huwa shakani.

Hapo vipigo ni jambo la kawaida kwa kuwa husaka ukweli wa jambo fulani au tatizo lililotokea. “Mimi mwenyewe niliwahi kupigwa mpaka nikateguka mkono nikiwa gereza la Segerea.

Siyo kwamba nilikataa kupekuliwa, bali askari walidai tu kwamba kuna simu mle gerezani, wakati ukweli ni kwamba, hakukuwa na simu. Ila tulipigwa ili tuseme ukweli,” amesema.

 “Mimi nilipigwa rungu, mkono ukateguka ila haukuvunjika, baadaye nikapewa panadol tu, mkono ukaja kupona wenyewe. Wengine walichanwa kwa kipigo.” Hata hivyo, anasema wazazi wao walikuwa wakija kuwasalimia gerezani kila wiki na kuwaeleza maendeleo ya kesi yao