Ewura yafanya tathimini kupata bei moja petrol nchi nzima

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza wakati alipokuwa akijibu maswali ya wabunge leo Jumatano Aprili 3, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima.

Dodoma. Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 3, 2024 na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo.

Gambo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja nchi nzima.

Akijibu swali hilo, Kapinga amesema Serikali kupitia Ewura inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima.

“Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi,”amesema Kapinga.

Amesema hivyo wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko.

Amesema tathimini  hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii.

Akiuliza maswali ya nyongeza, Gambo amehoji ni lini Serikali inategemea kumaliza changamoto hiyo ili wananchi waweze kupata kwa bei kama wanavyopata wenzao wa Dar es Salaam.

Pia amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa inatatua changamoto kama ilivyosema kwenye majibu ya swali la msingi.

Akijibu maswali hayo Kapinga amesema tathimini hiyo ilikuwa ni maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ambapo aliagiza kufanya tathimini hiyo kwa haraka sana ili kujua kama wanaweza kwenda kwa mfumo huo.

“Suala hili ni la kipaumbele na litakamilika hivi karibuni na tathimini hiyo itatueleza namna ambavyo tutatua changamoto zilizojitokeza kwa huko nyuma,”amesema.