Ewura yataka mitungi ya gesi kupimwa uzito

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekuja na mwarobaini wa kudhibiti wizi wa gesi kwa kuwaagiza wasambazaji wakubwa na mawakala  kupima uzito mitungi ya nishati hiyo kabla ya kuwauzia wateja.


Mbeya. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekuja na mwarobaini wa kudhibiti wizi wa gesi kwa kuwaagiza wasambazaji wakubwa na mawakala  kupima uzito mitungi ya nishati hiyo kabla ya kuwauzia wateja.

Kaimu meneja Ewura wa kanda hiyo, Muhiba Muhiba ameeleza hayo leo Jumanne Januari 26, 2021 wakati akitoa elimu kwa wajasiriamali na madereva.

Amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza nishati ya gesi isiyoendana na uzito na thamani ya fedha na kuwataka wananchi kuwa mabalozi ili kuthibiti uchakachuaji huo.

"Pia tumeagiza wasambazaji wakubwa wanaosafirisha nishati hiyo kuingiza nchini kuwa na leseni  zinazotolewa na Ewura na si vinginevyo…,ikiwa ni pamoja na kuwa na mikataba na mawakala kwa kuzingatia kanuni na sheria za Ewura ili kudhibiti uchakachuaji,” amesema.

Mkazi wa Mbalizi, Hamida Ramadhani amesema kwa kipindi kirefu wameuziwa nishati ya gesi kwa uzito tofauti na kuomba Ewura kudhibiti wizi huo.

"Kuna siku nimenunua gesi lakini inakwisha mapema tumechoshwa tunahitaji kama wadhibiti kulisimamie hilo kwani hakuna mawakala walio na mizani ya kupimia mitungi ya gesi "amesema.