Ewura yazitaka kampuni za mafuta kufungua vituo vya mafuta vijijini

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje

Muktasari:

  • Agizo la Ewura linatokana na kanuni mpya walizoandaa zinazotaka kampuni zinazoanzisha vituo vinne lazima kimoja kiwe kijijini. 

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na uhifadhi wa holela wa mafuta hasa maeneo ya viijijini, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeaandaa kanuni zinazotoa mwongozo kwa kampuni zote za mafuta nchini kuwa na vituo vijijini.


Hatua hiyo inalenga kukabiliana na madhara yanayojitokeza kutokana na watu hasa maeneo ya vijijini kuhifadhi majumbani petrol na dizeli kwa ajili ya biashara na matumizi.


Hali hiyo inatokana na kukosekana kwa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini hivyo kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata nishati hiyo.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje wakati akifungua kituo kipya cha mafuta cha Oryx kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam. 


Chibulunje alisema kanuni hizo tayari zimeshaandaliwa na muda wowote kuanzia sasa zitaanza kutumika lengi likiwa ni kuwasogezea huduma Watanzania.
Alisema nchini kuna jumla ya vituo vya mafuta 1,700 lakini idadi ya vilivyopo vijijini havizidi 200 jambo linalosababisha watu wanaoishi katika maeneo hayo kuhangaika kupata nishati hiyo.


“Kwa kanuni mpya tulizoziandaa, kila kampuni ya mafuta itakayokuwa na vituo vinne kimoja lazima kiwe kijijini. Lengo ni kuweka usalama wa watumiaji wa mafuta vijijini.

 
“Tunaposema Tanzania  ya viwanda ina maana huduma nyingi zitafika hadi vijijini. Magari yanakwenda kufuata mazao na malighali, wawekezaji nao wanakwenda huko  hivyo  lazima mafuta yapatikane,” amesema Chibulunje.


Katika hilo ameziasa kampuni za gesi kuhakikisha zinafanya uwekezaji mkubwa maeneo ya vijijini ili waishio huko waanze kutumia gesi katika matumizi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Oryx, Christopher Swart amesema kampuni hiyo inaendelea kufanya uwekezaji nchini na kuongeza idadi ya vituo vyake vya mafuta na gesi.


Amesema kituo kilichozinduliwa jana ni miongoni mwa vituo sita vilivyoanzishwa mwaka 2020.


“Pamoja na changamoto ya Covid 19, Oryx Tanzania imekuwa na mafanikio makubwa mwaka 2020 tumeongeza vituo na sasa hivi tunajivunia tuna vituo zaidi ya 50. Haya ni matokeo ya kazi nzuri na ushirikiano tunaopata kutoka kwa wateja wetu,” amesema Swart