Fahamu mchozo (ute ute) wakati wa ujauzito

Fahamu mchozo (ute ute) wakati wa ujauzito

Muktasari:

  • Uwepo wa mabadiliko mbalimbali wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida kutokea ikiwamo matiti kuvimba, mishipa ya veini kujaa, ngozi kututumka, kichefuchefu au kutapika na moyo kwenda kasi.

Uwepo wa mabadiliko mbalimbali wakati wa ujauzito ni jambo la kawaida kutokea ikiwamo matiti kuvimba, mishipa ya veini kujaa, ngozi kututumka, kichefuchefu au kutapika na moyo kwenda kasi.

Mabadiliko hayo huweza pia kuambatana na kutoka kwa mchozo ukeni, hali ambayo inaweza kumshtua mjamzito.

Kitabibu mchozo hujulikana kama “varginal discharge”, ni kimiminika cha ute ute unaotoka ukeni unaoweza kuonekana wakati wa ujauzito au katika hali ya kawaida.

Mchozo unaweza kuwa ni hali ya kawaida tu au ikawa ni tatizo la kiafya kutokana na harufu yake au namna ulivyo. Ute ute huo huwa umetengenezwa na majimaji ya njia ya uzazi na seli zilizokufa.

Kila mwanamke katika maisha yake anaweza kupata mchozo akiwa mjamzito au katika hali ya kawaida, mara nyingi huiona hali hiyo katika kitako cha nguo yake ya ndani anapokwenda kujisaidia. Mchozo huu unaweza kuwa ni kawaida kuwepo, kwani ni mbinu ya nyumba ya uzazi kutiririsha ili kujisafisha.

Ni kawaida kwa miezi ya awali ya ujauzito katika muhula wa kwanza kwa mjamzito, mchozo au ute ute huo kuongezeka kuliko siku za kawaida.

Mchozo huo huwa ni mzito usio na rangi wala harufu mbaya, unaweza kuongezeka zaidi kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha kichochezi cha Estrogen wakati wa ujauzito na mtiririko mwingi wa damu.

Inapotokea mchozo huo ukawa na harufu mbaya, kuwasha au hisia ya muunguzo wa moto huweza kuwa ni ishara ya uwepo wa uambukizi wa bakteria au fangasi wa njia ya uzazi kutokana na mabadiliko ya homoni.

Vile vile mchozo huo kuwa na rangi ya kijani, njano au kijivu ni moja ya kiashiria kingine cha uambukizi.

Pengine kwa kutokujua kwa baadhi ya wajawazito wanapoona dalili hizi huamua kujisafisha kwa njia zisizo sahihi, zikiwamo kemikali, manukato au sabuni kali na kuingiza ukeni.

Kufanya hivi si sahihi, kwani kuingiza vitu ukeni huweza kuharibu usawa wa tindikali ya eneo hilo na hivyo kuwapa nafasi zaidi bakteria kustawi katika njia hiyo baada ya kuharibu ulinzi wa uke ambao ni tindikali.

Njia inayokubalika kiafya ni kusafisha tu kwa maji tiririka yaliyo safi au kwa kutumia kitambaa safi kilicholowekwa katika maji safi ya vuguvugu.

Ni muhimu pia kwa mjamzito kufahamu kuwa mwishoni mwa ujauzito katika muhula wa mwisho anaweza kuona bonge la ute ambalo huwa na ukungu mweupe au pinki likiporochoka ukeni.

Hali hii ni ya kawaida, kwani huwa ule ute mzito unaokaa katika mlango wa uzazi kuzuia vimelea kupita kuelekea ndani ya nyumba ya uzazi.

Tukio la ute huu kutoka ghafla ni ishara ya kuanza kwa uchungu wa kujifungua kwa mlango wa uzazi kulegea ili kutoa nafasi mtoto kushuka.

Pia ute ute unaweza kutoka kiasi ukeni wakati wowote pale mjamzito anapopata mshtuko au mwili unapopata shinikizo katika maeneo ya tumboni.

Hivyo ni jambo la msingi sana kufahamu haya na kutoa taarifa kwa mtoa huduma aliye jirani nawe, ikiwamo daktari, muuguzi, mkunga wa huduma za afya au wa jadi kwa ajili ya kukupa ushauri sahihi.