Faida za kiafya mwanafunzi kuamka mapema
Wataalamu wa afya wanasema wanafunzi kama hawa pichani kuamka na kwenda shuleni mapema, kuna faida za kiafya na ni maandalizi ya maisha ya ukubwani. Picha na Makataba
Umewahi kuwashuhudia wanafunzi Alfajiri mapema wakiwa kweye usafiri kwenda shuleni? wengine wa umri mdogo wa madarasa ya awali, saa 11 Alfajiri wakiwa kwenye daladala au kwenye mabasi ya shule wakiitafuta elimu?.
Je? wale wanaoishi mbali na shule na kulazimika kutoka majumbani Alfajiri sana ili kuwahi vipindi? mazingira haya unaambiwa licha ya kuwa ni karaha kwa wazazi wengi, lakini ki afya ni tiba na yanamjenga mtoto.
Shule nyingi hasa za binafsi, mabasi ya shule yana ratiba ya kuanza safari saa 11:00 Alfajiri na mengine saa 11:30 kulingana na ruti, ingawa yapo baadhi mtoto anapitiwa baada ya muda huo hadi saa moja asubuhi.
Mmoja wa wazazi anasema alilazimika kuongea chemba na dereva wa basi la shule anakosoma mwanae ili kubadili ratiba ya kumchukua mtoto asubuhi.
“Nilikuwa nampa pesa kidogo, ili mradi aanzie kwingine na mwanangu awe wa mwisho kupitiwa nikiamiani itampunguzia hadha ya kuamka alfajiri sana, kabla ya kutumia mbinu hiyo, mtoto alikuwa akifuatwa saa 11:30,” anasema mzazi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Diana Harrison wa Dar es Salaam.
Dereva wa moja ya shule maarufu jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Saimon alisema muda wa kuchukua gari shuleni ni saa 10, tayari kuanza kupitia watoto na saa 10:30 jioni anakuwa amemshusha mtoto wa mwisho.
“Mtoto wa kwanza nampitia saa 11:20, wakati mwingine namsubiri hadi saa 11:30, ratiba ya ruti kwa mtoto wa kwanza kuchukuliwa ni hiyo hiyo haijawahi kubadilika, shuleni napaswa kufika saa 1:30, zaidi ya muda huo naonekana mzembe kazini,” anasema.
Ingawa baadhi ya shule inaelezwa ruti hupishana wiki hadi wiki, ikitokea mtoto wa kwanza kuchukuliwa wiki hii, basi wiki inayofuata anakuwa wa mwisho, vivyo hivyo kwenye kurudi jioni, ikitegemea a mazingira ya ruti hiyo.
Wazazi wahaha
Mmoja wa wazazi, Janeth Joseph anasema alilazimika kumuamisha mtoto kutokana na mazingira ya usafiri, japo shule ya awali ilikuwa ni nzuri na bora kitaaluma.
“Basi lilikuwa likimpitia kila siku saa 11:40, mtoto akifika kwenye basi anazungushwa nyumba zote hadi kufika shuleni amechoka wakati mwingine anasinzia, nikatafuta shule nyingine sasa anapitiwa saa moja asubuhi.
Mzazi mwingine, Wema Jeremiah anasema mwanawe tangu akiwa ‘baby class,’ alikuwa akipchukuliwa saa 11:30 Asubuhi, alipomuuliza dereva kwanini muda huo na shule ipo Kimara ambako si mbali na anapoishi, akamueleza anawahi ili kukwepa foleni.
“Mwanzo niliona kama mwanangu anapata tabu, kuna muda ili aamke ilikuwa tunabembelezana hasa miezi sita ya mwanzo shuleni, lakini sasa amezoea, hasumbui tena” alisema.
Martha Julius anasema tangu mwanawe akiwa baby class 2020, ratiba ya kufuatwa ni saa 11:30, akichelewa sana saa 11:40 au 45.
“Ameingia middle class, pre unit mwendo ni huo huo, kuna muda dereva anafika saa 11:15 anapiga simu hadi tunagombana, anataka akifika kituoni amkute mtoto, kama mzazi nilikuwa namuonea huruma mtoto, wakati mwingine naweka ‘ukauzu’ hadi saa 11:40 ndipo nampeleka,” anasema.
Jitwae Gamba anasema binti yake anasoma moja ya shule za Serikali iliyopo Posta, jijini Dar es Salaam na wao wanaishi Kawe ambako jiografia ya maeneo hayo si rafiki.
“Sikuweza kumhamisha, lakini nilitakiwa nimpe elfu mbili kila siku, nusu ya chakula na nusu ya nauli, kulikuwa na basi si rasmi la shule ambalo linawapitia, saa 11:00 alipaswa kuwa kituoni, amepitia kipindi kigumu kuna siku akiwa na mama yake walikabwa na vibaka,” anasema.
Ni tiba
Dk Nassor Matuzya anasema mtoto kwenda shuleni asubuhi sana si mateso wala adhabu, bali ni tiba na inamjengea mazoea hayo hata atakapokuwa mtu mzima.
“Ki afya aina tatizo, ili mradi tu awe ana lala mapema na kuamka mapema, anapoamka alfajiri na kupigwa na lile baridi liamsaidia kuimarisha mwili na akili pia, ndiyo sababu watu wanashauriwa kufanya mazoezi alfajiri,” anasema.
Anasema mbali n kuwa tiba, lakini kuamka Alfajiri kwa mtoto kuna mjengea mazoea, kwai kuna vitu vinafanyika katika jamii vinaweza kushangaza lakini vinakujenga.
“Unaweza kujiuliza hivi aliyeanzisha kusoma alikuwa akimaanisha nini? kwenye muda wa kufika shule pia, ni saa 1:00 au 1:30 asubuhi, utakapokuwa mtu mzima ni muda huo huo utatakiwa ufike kazini.
“Cha muhimu hapo ni kuzingatia mtoto analala muda gani, kama atalala saa 4 usiku halafu saa 10 Alfajiri anaamshwa kujiandaa kwenda shule haya ni mateso, lakini kama anaamka saa 10:30, basi mzazi ahakikishe saa 2:00 huyo mtoto anakuwa tayari amelala.
“Asilale chini ya saa 8, hii itamjenga hata atakapokuwa katika mazingira ya kazi, atazoea kuamka mapema na kulala mapema, japo kwa mazingira ya kawaida kuna wengine wataona kama ni adhabu lakini sivyo,” anasema.
Akitolea mfano kwa mwanafunzi ambaye yuko jirani na shule ambaye kengere ya kwanza ikilia ndiyo anaamka, ile ya pili ndipo anatoka nyumbani kukimbia shule kuungana na wenzake, anasema hiyo ina athari pia kwa mtoto.
“Kama amezoea kuamka saa moja, akipelekwa mazingira ambayo yatamlazimu aamke mapema zaidi lazima ataona ni magumu na wapo wengine wanashindwa kwa kuwa hakujengewa mazoea hayo tangu mwanzo, yule aliyezoeshwa hata huko baadae kazini hapati tabu.
“Ukimuona mtu anaingia ofisini saa moja au chini ya muda huo, wengi wao watakuwa wameyaishi maisha ya kuamka mapema na ikamjengea tabia hiyo, kwa mtoto anayesoma si mateso ni tiba na tabia ambayo inakuja kumjengea mazoea ambayo yatamjenga hata atakapokuwa mtu mzima katika mazingira ya kazi,” anasema.