Familia ya mwanamke tajiri Afrika inavyopitia msukosuko -3

Thursday October 14 2021
MWANAMKEPICC
By Luqman Maloto

Miaka 38 ya mamlaka, amri, ushawishi na nguvu ya kufanya kila kitu, tamati yake ilikuwa Septemba 2017. Baada ya hapo, zikaingia zama za kutaabishwa. Hii ndiyo simulizi ya Eduardo dos Santos na bintiye, Isabel. Mwanamke aliyewahi kutambulika mwenye utajiri mkubwa zaidi Afrika.

Kabla ya Septemba 2017, familia ya Eduardo dos Santos ‘Zedu’, iliweza kufanya kila kitu. Nani angethubutu kusimama katikati kuzuia mke au watoto wa Zedu wasifanye walichotaka Angola?

Tangu mamlaka ya nchi yalipotua mikononi mwa Rais wa sasa, João Lourenço ‘JLo’, familia hiyo imegeuka watangaji duniani. Wote wameamua kukimbia. Kwa kuanzia, baba yao amehamishia makazi yake Barcelona, Hispania.

Soma zaidi:Familia ya mwanamke tajiri zaidi Afrika inavyopitia misukosuko

Isabel, yeye makazi yake hayaeleweki kwa sasa. Wakati mwingine anaishi London, Uingereza, zipo nyakati anajitambulisha kama mkazi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Muhimu kwake ni kuwa hataki kurejea tena Angola, maana imeshageuka ardhi ngumu kwao.


Advertisement

Familia ya Zedu

Coreon Du mama yake anaitwa Maria Luisa Abrantes Perdigao. Watoto wa Zedu na mama zao kwenye mabano ni Isabel (Tatiana Kukanova), Zenu na Tchize (Filomena Sousa), Coreon Du (Maria Luisa), kisha wadogo wao watatu, Eduane Danilo, Joseana na Eduardo Breno ambao mama yao ni Ana Paula dos Santos.

Ana Paula alikuwa mwanamitindo na mhudumu wa ndege. Zedu alipomtupia jincho, alikamatika na kuanza kutoka naye kimapenzi kabla ya kufunga ndoa mwaka 1991. Wakati wanaoana, Ana alikuwa na umri wa miaka 28, Zedu 49 na Ana alikuwa tayari mjamzito.

Katika watoto saba wa Zedu, ni Coreon Du pekee aliyempata nje ya ndoa. Wengine wote, mama zao alifunga nao ndoa, kisha wakaachana kwa sababu mbalimbali. Ndoa ya kwanza ya Zedu ni ile aliyofunga Azerbaijan na Tatiana, mama wa Isabel.

Kipindi akiwa madarakani, Zedu alifanya kila alichotaka. Aliweza kulifanya Bunge kutunga sheria za kumruhusu kuchota fedha za umma alivyotaka, leo ameondoka madarakani, nyumbani hakukaliki. Si yeye wala watoto wake.

Alipokuwa madarakani, alianzisha cheo cha Waziri Mkuu na kumteua mdogo wake, Fernando da Piedade Dias dos Santos. Kisha akamteua kuwa Makamu wa Rais. Nani angemzuia?

Leo Fernando ni Rais wa Bunge la Angola, lakini hana uwezo wa kumsaidia kaka yake ili watoto wake wasisumbuliwe. Fernando alishindwa hata kuzuia mtoto wa kaka yake, Tchize, asifukuzwe ubunge wakati yeye ndiye mkuu wa Bunge.

Elewa hili; Afrika ilivyo kwa sasa ni kwamba ukiwa Rais unaweza kufanya chochote. Ukiondoka unaweza kutendwa chochote, inategemea na utashi wa atakayeingia madarakani baada yako. Rais mstaafu na watoto wake wapo uhamishoni. Aliyebaki (Zenu), ana kesi, haruhusiwi kutoka.

Isabel, mwanamke tajiri sana, hajulikani anaishi wapi kama makazi yake rasmi. Mara Uingereza, mara Ureno. Mwenyewe anadai nchi ya makazi yake ya kudumu kwa sasa ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), lakini mara kwa mara yupo Barcelona kwa baba yake. Anasema Angola si salama kwa maisha yake na familia yake. Yeye na mumewe, Mkongomani Sindika Donkolo, walisakwa mno na Serikali ya Angola ili waelekezwe kibla. Hata hivyo, Sindika alifariki dunia kwa ajali Oktoba 29, mwaka jana.

Wana fedha nyingi. Wana majumba na mali za kuwawezesha kuishi maisha ya daraja la kwanza kila nchi watakayo duniani, ila amani hawana. Ni kipindi hiki, pengine watoto wa Zedu wanatamani bora baba yao asingekuwa Rais. Pengine, Zedu anawaza bora angepatana na Savimbi miaka ile ya vita ya kiraia Angola na hata angempa Urais Savimbi kuliko alivyomwachia JLo. Wanapata tabu sana.

Ni simulizi ya Zedu, Rais aliyeliongoza taifa linaloshika nafasi ya tatu kwa uchumi mkubwa Kusini ya Jangwa la Sahara. Nchi yenye utajiri mkubwa mafuta. Inamhusu Isabel, mwanamke tajiri zaidi Afrika, akikadiriwa kuwa na utajiri wa dola 2.1 bilioni (Sh4.9 trilioni). Hiyo ni kwa mujibu jarida la kimataifa la utafiti na thamini za mali za watu, Forbes.

Utajiri huo unatajwa kuwa cha mtoto kwa ule alionao Zedu. Ripoti zinasema Zedu ana utajiri wa Dola 20 bilioni (Sh46 trilioni). Jumba lake la kifahari linalotazama bahari, Miramar, Luanda, lipo tupu. Limepooza.Advertisement