Familia ya mwanamke tajiri zaidi Afrika inavyopitia misukosuko

Tuesday October 12 2021
mwnaamketajiripic
By Luqman Maloto

Januari 19 mwaka jana, Jumuiya ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ), ilitoa ripoti ya uchunguzi jinsi Angola ilivyotafunwa na mwanamke tajiri zaidi Afrika, Isabel dos Santos. Ripoti hiyo ilipewa jina la “Luanda Leaks,” Luanda ndio Mji Mkuu wa Angola.

Walibainisha jinsi Isabel, alivyoanzisha kampuni mama ya Victoria Holdings, makao yake makuu yakiwa Kisiwa cha Malta. Baadaye Victoria Holdings ikawa mbia wa kampuni kubwa ya kutengeneza vito vya thamani, inayoitwa De Grisogono.

Mfanyabiashara Mcongoman, Sindika Dokolo na Kampuni ya Biashara ya Almasi Angola ya Sodiam, walitajwa kuwa wamiliki wa Kampuni ya De Grisogono.

tajiriiipicc

Sindika ni mume wa Isabel. Anayemiliki Victoria Holdings. ICIJ kupitia Luanda Leaks, waliitaja De Grisogono jinsi inavyochota rasilimali za umma Angola.

Januari 19, 2020, ICIJ waliitaja De Grisogono katika Luanda Leaks. Siku 10 baadaye, yaani Januari 29, 2020, De Grisogono, ikajitangaza kuwa mufilisi. Mengi kuhusu Isabel na mumewe, yalianza kuwekwa bayana baada ya Septemba 2017.

Advertisement

Ni kwa nini? Sababu ni moja tu; baba wa Isabel, Eduardo dos Santos ‘Zedu’, ndiye alikuwa Rais wa Angola. Kashfa ni kuwa kipindi Zedu alipokuwa madarakani, aliacha familia yake ijinufaishe kwa rasilimali za umma. Si kwa Isabel pekee, bali watoto wake wote.

Miaka 38 ya utukufu

Naam, miaka 38 ya mamlaka, amri, ushawishi na nguvu ya kufanya kila kitu, tamati yake ilikuwa Septemba 2017. Baada ya hapo, zikaingia zama za kutaabishwa. Hii ndio simulizi ya Zedu na bintiye, Isabel. Mwanamke tajiri zaidi Afrika.

Kabla ya Septemba 2017, familia ya Eduardo dos Santos ‘Zedu’, iliweza kufanya kila kitu. Nani angethubutu kusimama katikati kuzuia mke au watoto wa Zedu wasifanye walichotaka Angola? Nchi ikawa mali yao. Familia namba moja. The most powerful family in Africa.

Baada ya Septemba 2017, imegeuka familia inayoishi kwa mahangaiko na wasiwasi. Angola yao si taifa salama kwao. Watu wa familia ya Zedu, wamekuwa raia wa Angola wanaosakwa kwa tuhuma za uhalifu kuliko wengine wote nchini humo.

Kipindi Zedu akiwa Rais, aliweza kumkabili, kumdhibiti na hata kumuua mpiganaji roho ya paka, Jonas Savimbi, aliyekuwa anaongoza jeshi la uasi la Unita. Siku hizi Zedu hana ubavu wa wowote. Hakuna askari anayemtii. Haitwi tena Amiri Jeshi Mkuu.

Zedu alipotangaza kung’atuka baada ya kukaa madarakani miaka 38 (1979-2017), alidhani maisha yangekuwa rahisi. Madaraka ya nchi aliyaacha ndani ya chama chake cha MPLA. Halafu aliyeshika usukani ni kijana wake, Joao Lourenco ‘JLo’. Zaidi, JLo alikuwa Waziri wa Ulinzi chini ya Zedu. Shaka ingetoka wapi?

Matarajio ya Zedu yalikuwa kuacha uongozi wa nchi na Serikali lakini angeendelea kuwa kiongozi wa chama tawala, MPLA. Hilo halikuwezekana. Zedu aliiona nchi ngumu mara tu JLo alipochaguliwa kuwa Rais wa Angola. JLo alipoingia madarakani, alianza kwa kumfurusha Isabel, kwenye kampuni ya Sonangol, ambayo ni taasisi ya umma inayosimamia shughuli zote za uvunaji na uuzaji wa mafuta Angola.

Isabel ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Sonangol. Aliteuliwa na baba yake, Zedu, wakati akiwa madarakani.

Isabel ni mtoto wa kwanza wa Zedu. Alimpata na mwanamke wa Kirusi, Tatiana Kukanova. Zedu alilazimika kuachana na Tatiana ili kutimiza matakwa ya kuwa kiongozi mkubwa wa kisiasa Angola. Uraia wa Tatiana, ungemuwekea kauzibe.

Baada ya Baba wa Taifa la Angola, Agostinho Neto, kufariki dunia Septemba 10, 1979 kwa maradhi ya homa ya ini na saratani, Lucio Lara, ambaye alikuwa bosi namba mbili ndani ya MPLA, alikaimu urais wa Angola kwa muda, lakini aligoma kushika madaraka ya kudumu.

Lara akaendesha uchaguzi, Zedu akaingia madarakani mwaka 1979. Tatiana alimchukua Isabel wake, wakaenda kuishi Uingereza. Isabel alipokua, akarejea Angola. Zedu akampokea, mtoto wa kwanza tena!

Kuanzia hapo, Isabel akaibuka kuwa mfanyabiashara tajiri, kisha mwanamke tajiri kuliko wote Afrika. Utajiri ambao kwa miaka mingi ulihusishwa na uporaji wa mali za umma Angola. Kama haikutosha, Zedu alimteua Isabel kuwa Mwenyekiti wa Sonangol. JLo aliposhika madaraka akamtimua.

Isabel sio mtoto pekee wa Zedu aliyetemeshwa kazi serikalini baada ya JLo kushika mpini. Yupo pia Jose Filomeno dos Santos ambaye Zedu alimpata na mwanamke raia wa Angola, Filomena Sousa.

Jose Filomeno ‘Zenu’ ni mtoto wa kiume wa kwanza wa Zedu. Mwaka 2012, Zedu alimteua Zenu kuwa Mwenyekiti wa Mfuko Mkuu wa Uwekezaji (FSDEA). Mfuko unaosimamia mali nyingi za umma. JLo baada ya kuingia madarakani, alimpiga chini Zenu.

Haitoshi, Zenu baada ya kung’olewa FSDEA, alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha, kujitajirisha kwa njia batili na kushiriki uhalifu wa mipango. Alibainika kuhamisha fedha, dola 500 milioni (Sh1.2 trilioni) kwenye akaunti yake katika benki moja ya Uingereza.

Zenu alikaa mahabusu mwaka mmoja na miezi sita, kabla ya kuachiwa Machi mwaka jana. Fedha hizo, dola 500 milioni, zilirejeshwa Benki Kuu ya Angola.

Kwa Zedu na familia yake. Julai 2017, kabla hata uchaguzi kufanyika, Zedu alisafiri kwenda Barcelona, Hispania mara mbili. Taarifa iliyotolewa ni kwamba alikwenda kwenye matibabu. Septemba 2017, kipindi cha makabidhiano ya uongozi, Zedu alisafiri kwenda Barcelona.

Itaendelea na simulizi hii kesho

Advertisement