FCS yatoa Sh4 bilioni kwa asasi 80

Muktasari:

Mkurugenzi mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga amezitaka asasi hizo kutumia ruzuku hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaonya watakaofanya ubadhirifu.

Dodoma. Taasisi ya Kuhudumia Asasi za Kiraia (FCS) imetoa Sh4 bilioni kwa wadau wa asasi 80 ikiwa ni mkakati wa kupunguza umaskini na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Fedha hizo zitakazotumika kwa miaka miwili zimetajwa kuyapa kipaumbele maeneo ya kimkakati kama maji, kilimo, elimu na afya.

Katika hafla iliyofanyika leo Agosti 15, 2022 jijini hapa, wadau hao wametia saini mkataba wa kutumia ruzuku hiyo katika malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza katika mafunzo ya utumiaji wa ruzuku hiyo Mkurugenzi mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga amewataka wadau hao kutumia ruzuku walizopewa kwa malengo yaliyokusudiwa kwani kuna baadhi yao wamekuwa wakifanya ubadhirifu.

Amesema kwa miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na ubadhirifu wa asilimia 5 hadi 6 ya ruzuku hivyo kuahidi kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya ubadhirifu huo.

“Kazi yetu ni kushirikiana na Serikali kwa kuongeza nguvu wakati pale watakapoelemewa, sasa ikiwa tunapata fedha na kutumia tofauti tujiandae kukumbana na mkono wa sheria.

 “Naomba hizi ruzuku zikatumike ipasavyo ndio maana tumeandaa mafunzo makusudi msiseme hamkufundishwa”amesema Kiwanga.

Mmoja wa wadau aliyepata ruzuku hiyo, Bernadetha Choma ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Tanzania women for Self ameeleza kwa upande wake kuwa ruzuku hiyo itawasaidia wakazi wa Mkinga Mkoani Tanga ambao wanakumbana na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.