Figisu zaibuka uchaguzi TLS

Figisu zaibuka uchaguzi TLS

Muktasari:

  • Baadhi ya wanachama wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) wamepeleka malalamiko kwa msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho, wakidai kuwepo ukiukwaji wa taratibu unaofanywa na kundi moja wapo la mgombea urais. 

Dar es Salaam. Wakati wanachama wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) wakianza kufanya uchaguzi kesho, baadhi ya wanachama wamewasilisha malalamiko yao kuhusu uchakachuaji wa orodha ya wapigakura.

Kesho Mei 27, uchaguzi mkuu wa Rais wa TLS, makamu wa Rais na mweka hazina wa chama hicho unafanyika jijini Arusha, ambapo baadhi ya wanachama wamewasilisha malalamiko hayo kwa kamati ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mtendaji Mkuu wa TLS iliyosainiwa pia na walalamikaji watatu; Frank Chundu, Hekima Mwasipu na Edson Kilatu, inaeleza kwamba orodha ya wapigakura imewahusisha mawakili ambao hawana sifa za kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Pia, wamesema orodha hiyo imewahusisha mawakili ambao wamepewa mamlaka ya kushuhudia viapo tu, ambao kimsingi wanafanya kazi kwenye taasisi za umma.

Walalamikaji hao wamebainisha kwamba baadhi ya mawakili wamepewa vibali vya kuwapigia kura wenzao (proxy) zaidi ya viwili akiwemo mgombea urais anayetetea nafasi hiyo, Profesa Edward Hoseah ambaye ana vibali zaidi ya viwili.

“Masharti ya kuwa mwanachama yameainishwa katika kifungu cha 6(a) (b) (c) cha Sheria ya Chama cha Mawakili cha Tanganyika. Ili kukidhi masharti ya uanachama kwa mujibu wa tafsiri ya kanuni ya 2 ya kanuni za uchaguzi, ni lazima mwanachama huyo awe amehuisha leseni yake.

“Hata hivyo, kwa mujibu wa mwongozo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Novemba 27, 2020, kifungu cha 4(1) kimekataza mawakili katika utumishi wa umma kupewa leseni za kufanya kazi ya uwakili kama mawakili isipokuwa kwa sababu maalumu,” inaeleza barua hiyo.

Katiba barua yao, walalamikaji hao wameambatanisha barua hiyo na orodha ya majina 120 ya mawakili ambao hawana sifa ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Charles Rwechungura amekiri kupokea malalamiko hayo na wanayafanyia kazi.

“Ni kweli tumepokea malalamiko hayo, na muda huu tunazungumza nipo kwenye kikao tukijadili suala hilo,” alisema Rwechungura.