Furaha ya matokeo kidato cha nne ilivyokatisha maisha ya mwalimu

Mwalimu, Gaudence Aloyce enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Mwalimu wa shule ya Sekondari ya Musoma Ufundi iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara amefariki dunia kwa kugongwa na gari muda mfupi baada ya kukutana na waalimu wenzake kwaajili ya kupongezana baada ya shule yao kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne.

Musoma. Mwalimu wa shule ya Sekondari ya Musoma Ufundi iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara Gaudence Aloyce (33) amefariki dunia kwa kugongwa na gari muda mfupi baada kumaliza sherehe ya kupongezana na waalimu wenzake kufuatia shule yao kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne 2022.

 Mwalimu huyo pamoja na wenzake walikutana kupongezana baada ya shule yao kupata ufaulu wa 1.7 (GPA) kwenye matokeo yaliyotangazwa na baraza la mitihani hivi karibuni.

Mkuu wa shule hiyo, Magita Nyangore amesema Aloyce alifariki Januari 29, 2023 kwenye barabara ya Nyerere eneo la Baruti mjini Musoma wakati akirudi nyumbani.

"Alipofika maeneo yale akiwa anaendesha pikipiki yake ghafla basi lililokuwa mbele yake lilikata kona kuingia kituo cha mafuta na akajikuta akiligonga kwa ubavu na kupelekea kuanguka na kufariki pale pale." alisema Nyangore na kuingeza,

"Tulikutana pale container jioni kwaajili ya kuchoma kuku maana tumepata daraja la kwanza 94, daraja la pili 16, daraja la tatu 5 na daraja la nne 4 na baada ya hapo tukatawanyika kika mtu akaendelea na shughuli zake lakini baadaye kwenye saa 2.30 usiku nikapigiwa simu kuwa mwalimu amepata ajali."

Nyangore amesema kuwa wanafunzi 80 kati ya 119 waliofanya mtihani wa kidato cha nne shuleni hapo wamepata alama A kwenye somo la bailojia ni somo ambalo alikuwa akifundisha mwalimu huyo na kwamba ufaulu huo umeongezeka kutoka alama A 71 za somo hilo shuleni hapo mwaka 2021.

"Alikuwa ni mahiri kwenye somo la bailojia ndio maana mwaka juzi tulipata A 71 na sasa zimezidi kuongezeka hadi kufika 80." Amesema Nyangore.

Mkuu wa idara ya elimu maalum shuleni hapo, Rosena Anthony amesema kuwa mbali ya kuwa mwalimu wa baiolojia lakini marehemu Aloyce enzi za uhai wake alikuwa ni mwalimu wa lugha ya alama pia.

"Alikuwa ni mwalimu wa elimu maalumu upande wa lugha ya alama kwa wanafunzi viziwi na ukiangalia matokeo ya mwaka jana kulikuwa na wanafunzi wengi tu wa elimu maalumu walifaulu vizuri." Alisema Rosena.

Baadhi ya wanafunzi wamemuelezea mwalimu huyo kuwa alikuwa na bidii kwenye somo lake huku akitaka kila mwanaufunzi darasani kwake aweze kulielewa somo la biolojia.

"Kwanza alikuwa akiingia darasani lazima mtacheka maana alikuwa ni mcheshi sana lakini pia alikuwa akitumia hata muda wake wa ziada kutufundisha lengo lake lilikuwa ni kutaka kila mwanafunzi darasani kwake aweze kuelewa vizuri somo lake." amesema Frank Hamisi wa kidato cha sita

"Alikuwa radhi kutumia muda wake wa mapumziko kwaajili ya wanafunzi anatuchukua na kwenda 'lab' kwaajili ya masomo ya ziada tena bila malipo, mwalimu alikuwa mwenye upendo sana." ameongeza Samson Mpelwa wa kidato cha sita.