Gambo: Ulikuwa uporaji shughuli ya kufunga maduka ya kubadilisha fedha za kigeni

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (CCM),  Mrisho Gambo amesema shughuli ya kufunga maduka ya kubadilishia fedha za kigeni iliyofanyika nchini takribani miwili iliyopita, ilikuwa ni uporaji wa kuumiza watu.


  

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM),  Mrisho Gambo amesema shughuli ya kufunga maduka ya kubadilishia fedha za kigeni iliyofanyika nchini takribani miwili iliyopita, ilikuwa ni uporaji wa kuumiza watu.

 Akizungumza jana Jumatatu Juni 14, 2021 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti kuu ya Serikali, Gambo amedai mchakato huo ulikuwa kama nia ya baadhi ya watumishi wa Serikali kutaka wafanye wao biashara hiyo.

Novemba 20, 2018 maduka zaidi ya 20 yalifungwa jijini Arusha baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Serikali wakishirikiana na vyombo vingine vya dola.

Aprili, 2021 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga alisema kati ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni 87 yaliyofanyiwa ukaguzi jijini Dar es Salaam, 82 yalikutwa na viashiria vya utakatishaji wa fedha.

Katika maelezo yake,  Gambo ambaye amewahi kuwa mkuu wa Mkoa Arusha amedai Serikali ilikuwa ikipandisha viwango vya mitaji kwa lengo la kutaka wafanyabiashara washindwe lakini walipoendelea kufanya biashara zao waliona hakuna namna zaidi ya kuvamia.

"Mlichukua fedha zao, magari, viwanja vyao na mali nyingine watu wakabaki hawana kitu hivi lengo la Serikali ilikuwa nini," amesema Gambo.

Gambo amezungumzia pia sekta ya Utalii akisema imeachwa kabisa bila kuwekewa mkakati katika bajeti jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa nchi.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kubuni mbinu ya kuvutia ili kuongeza watalii badala yake imefikiria kuongeza tozo inayoweza kusababisha watalii kupungua nchini.

"Hii bajeti imeacha kabisa kutaja sekta ya utalii, wenzetu wanafikiria kuvutia watalii sisi tunawaza kuongeza tozo, mnawaza nini nyie," amehoji Gambo.

Ametolea mfano wa kupungua kwa watalii kwamba kumesababisha baadhi ya wawekezaji kupunguza gharama kwenye mahoteli yao kutoka Dola 200 za Marekani hadi Dola 100.