GGML yatoa msaada wa magari manne Veta Mwanza

Muktasari:

  • Magari hayo ni muendelezo wa msaada wa kampuni ya GGML kwa taasisi mbalimbali nchini katika kuzisaidia kuetekeleza majukumu yake ya kila siku.

Dar es Salaam. Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa msaada wa magari manne aina ya Toyota Land Cruiser kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (Veta) tawi la Mwanza.

Magari hayo ni muendelezo wa msaada wa kampuni ya GGML kwa taasisi mbalimbali nchini katika kuzisaidia kuetekeleza majukumu yake ya kila siku.

Akizungumza leo Mei 26 katika hafla fupi ya makabidhiano ya magari hayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti Geita Gold Mining Limited anayeshughulikia miradi endelevu kwa nchi za Tanzania na Ghana, Simon Shayo amesema msaada huo umetolewa muda muafaka.

“Tumeunga mkono juhudi za Veta kwasababu kwa kiasi kikubwa wanafunzi wanaotoka Veta ni wanafunzi wa kiutendaji ambao unamfanya mtu akitoka akafanye kile kitu ambacho amejifunza,” amesema.

Kuhusu mafunzo ya udereva na ufundi wa magari, amesema kuna changamoto ya ujuzi mdogo wa watu wanaotumia vyombo vya moto yakiwemo magari.

“Kwa hiyo mtu akipitia mafunzo kama haya ya Veta akitoka hapo atakuwa dereva bora zaidi.

“Tumefadhili karibu watu 130 kutoka kwenye jamii inayotuzunguka na wameajiriwa kwenye migodi kama mafundi wakubwa ikiwa ni mwendelezo wa kuongeza ajira kwa watanzania,” amesema. 

Amesema tangu mwaka 2006 kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imekuwa ikishirikiana vizuri na VETA kwa kusomesha vijana 130 katika mafunzo jumuishi ya ufundi katika madini.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu Mkurugenzi Mkuu wa Veta Kanda ya Ziwa, Charles Kaugele ameipongeza GGML kwa msaada huo akisema utasaidia pia kutoa mafunzo kwa vitendo wanafunzi wanaosomea udereva chuoni hapo.