Ghala la korosho lateketea Mtwara

Ghala la Kenoshukuru  linalo endeshwa na kampuni ya Synar Enterprises likiwa linaungua moto leo moto ambao ulianza jana usiku. Picha Florence Sanawa

Muktasari:

  • Zaidi ya tani 120 za korosho zimeteketea  kwa moto wilayani Nanyumbu katika ghala la Kenoshukuru linaloendeshwa na kampuni ya Synar Enterprises

Mtwara. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mtwara, limetoa taarifa ya awali ya kuungua kwa jengo lililokuwa likitumika kama ghala la kuhifadhia korosho la Kenoshukuru.

Akitoa taarifa hiyo kwa simu wakati anazungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 1, 2023,  Kamanda wa jeshi hilo Mrakibu Msaidizi, Daniel Myalla amesema kuwa walipokea taarifa za kuunga kwa ghala hilo saa nne usiku.

Amesema kuwa baada ya kupata taarifa askari wa jeshi hilo walifika katika eneo hilo na jitihada za kuuzima moto huo hazikufanikiwa kwa kuwa ulikuwa umeshatanda.

“Askari wetu walifika mapema baada ya taarifa na kukuta moto ukiwa umetanda eneo karibu lote  hali ambayo ilionyesha kuwa taarifa zilichelewa, ghala  limeathirika kwa zaidi ya asilimia 95, tunafanya tathmini ili kujua thamani halisi za bidhaa zilizoteketea katika eneo hilo” amesema Myalla.

Nae Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Masasi na Mtwara Cooperative Union (Mamcu), Siraji Mtenguka  amesema kuwa takribani tani 125 za korosho iliyokwisha kununuliwa, zimeteketea kwa moto huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Dr Steven Mwakajumilo amesema kuwa baada ya ghala hilo kuungua ameunda kamati ndogo ambayo itachunguza chanzo cha moto huo.

Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahya Mhata ambaye ni mmiliki wa ghala hilo amesema kuwa jengo hilo ni lake na hulitumia kwa ajili ya biashara ambapo  kwa mujibu wa taarifa alizopata jengo hilo limetekea na vyote vilivyomo ndani. 

“Nikiwa kama mmiliki  wa jengo hilo ambalo nililikodisha huo ni msiba ile ni nyumba yangu ya biashara imeungua nimejenga kwa gharama, ile ni hasara kwangu siwezi kujua nini kilikuwepo ndani kwa kuwa mimi ni mmiliki wa jengo lakini waliokuwa wakiendesha ghala ni wengine,” amesema Mhata.

Mwananchi ilimtafuta aliyekuwa analiendesha ghala hilo, Daiz Ibrahim ambaye amesema kuwa alikuwa safarini hana taarifa kamili  ya korosho zilizoteketea katika ghala hilo linalomilikiwa na kampuni yao.