Ghorofa laporomoka Moshi, watano wafariki

Baadhi ya wananchi wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiondoa vifusi kwenye jengo la ghorofa mbili lililoanguka na kuua watu watano katika kijiji cha Sembeti, Marangu wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

Watu watano wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na jengo la ghorofa mbili, katika kijiji cha Sembeti, Marangu wilayani ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Moshi. Watu watano wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na jengo la ghorofa mbili, katika kijiji cha Sembeti, Marangu, wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 19, 2022, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abass Kayanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

"Ni kweli wamekufa watu watano na wengine wameokolewa na majeruhi wapo katika hospitali ya Marangu kwa matibabu zaidi," amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani hapa, Jeremiah Mkomagi amesema ghorofa hilo lilikuwa likiendelea kujengwa na taarifa walizozipata kulikuwa na mafundi na vibarua wapatao 30.

Amesema ghorofa hilo lilianguka Desemba 18 usiku wa saa mbili kuelekea saa tatu wakati mafundi na vibarua hao wakiendelea na kazi ya kumimina zege.

"Baada ya kufika hapa tuliambiwa kulikuwa na watu 30 waliokuwa wakiendelea na kazi ya ujenzi, jitihada za uokoaji ziliendelea ambalo watu watano waliondolewa kwenye eneo hili wakiwa tayari wameshafariki, 9 ni majeruhi ambao wameelezwa hospitali ya Marangu na 16 waliokolewa bila kupata madhara yoyote," amesema.

Kamanda Mkomagi amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha jengo hilo kuanguka ni kujengwa katika kipindi kifupi ambapo ndani ya wiki tatu tatulilikuwa likijengwa chini ya viwango na halikuzingatiwa utaalam.

"Uchunguzi wa awali unaonyesha jengo lilijengwa ndani ya muda mfupi na halikufuata utaratibu wa ujenzi na nondo  zilizotumika ziko chini ya kiwango," amesema Kamanda Mkomagi


Kamati yaundwa kuchunguza

Kufuatia kuanguka jengo hilo, Serikali mkoani Kilimanjaro imeunda kamati maalumu ya kuchunguza ajali hiyo ambayo imeseababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine tisa.

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Willey Machumu amesema tayari mkoa umeunda kamati ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Machumu amesema endapo itabainika kukiukwa kwa taratibu hatua za kisheria zitachukuluwa kwa wahusika.

"Tumeunda kamati kuchunguza sababu za jengo kuanguka  kuona kama kulikuwa na kibali na taratibu za ujenzi zilifuatwa, lakini pia kuona kama lilikuwa likisimamiwa na mhandisi ambaye ana ujuzi wa kutosha, lakini pia kamati hiyo itaangalia vifaa vilivyotumika kama vilikuwa na ubora unaostahili" amesema Machumu.