Gwajima aanza mikakati kupambana na ukatili wa kijinsia nchini

Saturday January 22 2022
mkakatipic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Wakati vitendo vya ukatili wa kijinsia vinazidi kuongezeka nchini Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum, Dk Dorothy Gwajima ametaja jitihada sita ambazo wizara yake imeanzisha ili kupambana na hali hiyo.

Pamoja na hayo ametoa agizo kwa vyuo vya elimu ya juu na kati vipatavyo 512 kuanza kupitia mwongozo wa uanzishaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati ya jinsia kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kudhibiti na kutokomeza ukatili vyuoni.

Waziri Gwajima ameyasema hayo leo Januari 22, 2022 wakati akizindua dawati la jinsia katika Taasisi za elimu ya juu na kati, hafla iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA).

Amesema katika kutekeleza mpango huo Serikali imechukua jitihada mbalimbali za kukabiliana vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya ukatili kwa kutumia njia mbalimbali.

“Jitihada hizi zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa vyombo husika na kwa kipindi cha mwaka 2020/21 jumla ya matukio 20,025 ya ukatili yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 18,270 yaliyoripotiwa kwa mwaka 2019/20,” amesema.

Advertisement

Dk Gwajima amesema madawati ya jinsia yanayoshughulikia mashauri ya ukatili shidi ya wanawake na watoto 420 yameanzishwa katika vituo vya polisi na madawati 153 katika jeshi la magereza yaliyowezesha wananchi kutoa taarifa.

Amesema wameunda na kuimraisha kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, kata na kwenye baadhi ya mtaa, vijiji na vitongoji ambapo hadi sasa kamati 18,186 zimeanzishwa nchini.

“Vituo vya mkono kwa mkono (one stop centres) vimeanzishwa ambavyo hutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia. Mpaka sasa tunavyo vituo 14 vinavyotoa huduma hizo kwenye baadhi ya hospitali hapa nchini,” amesema.

Hata hivyo amesema kuna kampeni kadhaa zimeanzishwa pamoja na kuongezeka kwa huduma za msaada wa sheria kutokana na kutungwa kwa sheria ya msaada wa kisheria Na. 1 ya mwaka 2017.

“Sheria hii imewezesha makundi maalum wakiwemo wanawake na watoto kupata haki zao katika vyombo vya utoaji haki. Kwa sasa tunao wasaidizi wa kisheria 4,195,” amesema Waziri Gwajima.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Telnolojia, Omary Kipanga amesema madawati hayo yataambatana na mradi wa O3 Plus utakaoleta manufaa makubwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kati ikiwemo upatikanaji mwongozo kitaifa wa uanzishaji, uendeshaji wa dawati la kijinsia kwa elimu ya juu.


Advertisement