Hapi awachomea vigogo Bunda Tamisemi

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa wamewasilisha maombi katika Ofisi ya Rais Tamisemi ili baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini waondolewe katika nafasi zao kwa maelezo kuwa hawatoshi.


Bunda. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa wamewasilisha maombi katika Ofisi ya Rais Tamisemi ili baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini waondolewe katika nafasi zao kwa maelezo kuwa hawatoshi.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Isanju katika halmashauri hiyo, HapiĀ  amezitaja idara ambazo zimekuwa ni kikwazo kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwa ni pamoja na idara ya Ununuzi, Mpango na Fedha huku akitoa muda wa saa 48 kupewa majina ya wakuu wengine aliosema ni kikwazo.

"Hii halmashauri lazima ifumuliwe maana hapa kuna ugonjwa lazima tuutibu na tiba yenyewe ni kuwaondoa wanaotuchelewesha hapa kuna ubinfasi na uzembe wa hali ya juu na wanaoumia ni wananchi na tatizo lipo kwa viongozi wa halmashauri," amesema Hapi


Hapi amefikia hafua hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa mradi huo wa kituo cha afya unatekelezwa kwa kusuasua kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kukosekan kwa vifaa vya ujenzi katika mradi huo ingawa fedha zilipokelewa tangu mwezi Septemba mwaka jana.

Awali fundi anayetekeleza mradi huo, Robert Mwijarubi amesema kuwa ujenzi huo umesimama kutokana kukosewa kwa vifaa ambavyo awali vililetwa lakini ikabainika kuwa vifaa hivyo sio sahihi

"Wamekwenda kubadili nondo mjini kwa hiyo tunasubiri hadi watakapoleta japo nondo hizo zimerudishwa mjini yapata wiki moja sasa," amesema.

Hapi amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo vilivyopokea fedha mapema lakini hadi sasa ujenzi bado upo katika hatua ya msingi huku akisema kuwa ni aibu kwa mradi huo kuwa katika hatua hiyo ilhali fedha zimepokelewa yapata miezi minne sasa.

"Nina mifano mingi sana hapa Bunda, mmenisumbua kwenye mradi wa madarasa ya uviko19, mradi wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri na miradi mingine mingi sasa nimechoka na nimegundua tukicheka na nyani tutavuna mabua" amesema

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Nassari amesema kuwa halmashauri hiyo imekuwa na shida kwenye utekelezaji wa miradi na kusema kuwa watumishi hao wanekuwa na tabia ya kujinufaisha binafsi huku miradi ikishindwa kutekelezwa.

Amesema kuwa katika kipindi alichokaa wilayani humo amegundua kuwa wapo baadhi ya wazabuni wamekuwa wakipewa fedha kwaajili ya kununua vifaa lakini badala ya kununua vifaa hivyo fedha hizo wamekuwa wakizitumia kwa shughuli zao binafsi pamoja na baadhi ya watumishi.

"Nashukuru mkuu ametoa maelekezo na tayari tuna orodha ya wafanyakazi ambao ni kikwazo na hili la kufumuliwa halmashauri halikwepeki, tunahangaika sana kwenye miradi maana kuna watu hapa wao kazi yao ni kuangalia mianya ya upigaji," amesema Nassari.