Hatua kwa hatua sakata la kina Mdee walivyomwagwa

Saturday May 14 2022
mdeepic
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Unaweza kusema kwa uhakika kuwa wamemwaga na hivyo ndoa ya wabunge 19 wa viti maalumu na Chadema imefika mwisho.

Hii ni baada ya kikao cha juu cha maamuzi kuhusu masuala ya kinidhamu kutupilia mbali rufaa ya wabunge hao kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwafukuza uanachama Novemba 27, 2020.

Ulikuwa usiku mnene juzi katika mkutano wa Baraza Kuu la Chadema uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam, pale wajumbe walipopiga kura nyingi za kubariki kufukuzwa kwao.

Uamuzi hao, licha ya kutarajiwa na wanachama wengi wa Chadema, haukutarajiwa na wabunge hao na Halima Mdee, kiongozi wa wabunge hao na aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha alisema:

“Kilichofanyika pale ni uhuni wa kiwango cha hatari. Hata Mbowe mwenyewe anajua.

“Huwa nakwepa kuzungumza maneno makali kwa sababu naheshimu viongozi wangu, lakini sikujua kama Chadema kunaweza kufanyika uhuni kwa kiwango hicho.”

Advertisement

Hata hivyo, Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema alipoulizwa kuhusu madai ya Mdee alijibu kuwa “Baraza Kuu limekaa leo (juzi) na walikuwa mashuhuda na wameona uamuzi wa wajumbe, sasa wakilalamika uamuzi ulifanyika kabla, hao wajumbe walikuwa wapi. Wajumbe wamekuja leo na wamefanya uamuzi wakishuhudia na kura zimepigwa mbele yao, waache mambo ya ‘kihuni,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema tayari uamuzi wa kuwafukua ulishafanywa na Kamati Kuu tangu Novemba 2020, hivyo Baraza Kuu limebariki tu.

Baada ya uamuzi huo, haraka chama hicho kilianza mchakato wa kulifahamisha Bunge juu ya uamuzi kwa hatua zaidi.

Jioni Mrema, mkurugenzi wa mawasiliano, itikadi, uenezi na mambo ya nje wa chama hicho alisema jana jioni kuwa barua kwenda Spika imeshafika Dodoma kwa njia ya mtandao kupitia barua pepe za ofisi ya Spika na Bunge pamoja faksi.

Vilevile, alisema njia ya kawaida mjumbe maalumu wa Chadema alikuwa njiani kuelekea Dodoma kuwasilisha barua hiyo pia kwa mkono.

“Tumetuma nakala pia katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisema Mrema.

Hali ilivyokuwa

Wabunge hao 19 wakiongozwa na Mdee waliwasili katika eneo la ukumbi majira ya saa 6 mchana wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Coaster wakisindikizwa na mabausa waliovalia sare nyeusi.

Hata hivyo, wakati wabunge hao waliruhusiwa kuingia na kupewa eneo maalumu la kukaa, timu ya ulinzi wa chama iliwazuia walinzi wao kuingia.

Wakati ajenda ya rufaa za wabunge hao ilikuwa ya mwisho, mkutano huo ulianza na ajenda zake nyingine, ikiwemo kujadili hali ya siasa nchini na taarifa ya kamati kuu iliyowasilisha taarifa za hali ya gharama za mafuta.

Pia walijadili mikakati na mipango ya Chadema ya miaka mitano, mpango kazi wa mwaka 2022/23, maandalizi ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na uteuzi wa bodi ya wadhamini na mengineyo ambayo bado hayajatolewa taarifa.

Wakati ajenda ya kina Mdee ikiwadia kujadiliwa majira saa nne usiku, kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe, hali ya ukumbi ilikuwa ya utulivu na wajumbe walikuwa na shauku kuhusu jambo hilo lililoshuhudiwa na naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza.

Inaelezwa kabla ya kuwaita wabunge hao mmoja baada ya mwingine, Mbowe alitoa angalizo kwa wajumbe hao akiwataka kutozomea wala kushangilia kwa lolote pindi wabunge hao watakapoanza kuingia ndani ya ukumbi huo.

Ilipofika saa 4 usiku, wa kwanza alikuwa Asia Mohamed aliyeingia ukumbini akisindikizwa na walinzi wa chama saa 4:18 usiku.

Wa pili aliitwa Agnester Lambert na wengine, huku wa mwisho akiitwa Sophia Mwakagenda.

Taarifa zinasema walitakiwa kusoma kuthibitisha barua ya rufaa kwa wajumbe wa Baraza Kuu kama ilikuwa sahihi.

Wakata wabunge hao wakiingia walitumia lango walilokuwa wanatumia viongozi wakuu wa Chadema na kutokea mlango wa nyuma.

Baada ya kumaliza hatua hiyo, saa 5:36 usiku wabunge hao wote waliitwa kwa pamoja kwenye ukumbi huo na kuketi eneo maalumu mbele ya wajumbe.

Wakiwa ukumbini, Katibu Mkuu John Mnyika alisoma mwenendo wa shauri lao na utetezi wa hoja za Kamati Kuu dhidi ya hoja za rufaa zao.

Baada ya Mnyika kusoma mwenendo huo, Mbowe alitoa fursa kwa kina Mdee na wenzake kusema chochote, lakini hawakutaka kuzungumza chochote.

Kura za wazi

Hatua iliyofuata ilikuwa kila kanda za chama hicho kuhakiki wajumbe wake waliopaswa kusimama kwa makundi kwa kadiri walivyoongozwa na Mbowe.

Katika kura hizo, walitakiwa ama kuunga mkono uamuzi wa kamati wa kuwavua uanachama, kutounga mkono au kutofungamana na upande wowote.

Baraza Kuu liliamua mchakato wa kura uwe wazi, kutokana na tuhuma za baadhi ya wajumbe kupewa fedha na baadhi ya wabunge hao.

Kura hizo zilishirikisha wajumbe wa Baraza Kuu 423, kati yao 413 sawa na asilimia 97.6 walikubaliana na uamuzi wa kamati kuu ya Chadema, wa kuwavua uanachama, watano sawa na asilimia 1.2 hawakukubaliana na uamuzi wa kuwafukuza, huku wasiofungamana na upande wowote wakiwa watano, sawa na asilimia 1.2.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa ukumbi ulilipuka kwa shangwe na vigelegele, kisha Mdee na wenzake wakatoka nje ya ukumbi wakitumia lango la wageni mashuhuri kuondoka.

Madai ya rushwa

Kwa siku kadhaa kabla ya kikao kulikuwa na madai za baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu hilo, wakiwemo viongozi wa mikoa na wilaya wakidaiwa kupewa kati ya Sh50,000 hadi Sh100,000 ili kuhakikisha wabunge hao hawafukuzwi.

“Ni kweli kuna fedha zilitembezwa na kuna viongozi wetu walikamatwa na miamala ilithibitika. Ndiyo maana Mbowe aliwaonya waliohusika akitaka hatua stahiki zichukulie,” alidai mmoja wa wajumbe.

Hata hivyo, mmoja wa wabunge waliovuliwa uanachama, Salome Makamba alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema “ni madai ya uhuni yaliyolenga kutuchafua kwa wajumbe wa Baraza Kuu, mwenye uthibitisho wa hili afuate taratibu za kisheria ili hatua zichukuliwe.

“Rushwa ni jinai, unapomtuhumu mtu kwa kosa la rushwa bila uthibitisho ni kosa… kama kuna uthibitisho watumie kanuni za chama au sheria kuchukua hatua,” alisema Salome.

Baada ya wabunge hao kuondoka, Mnyika aliwashukuru wajumbe akisema “baada ya kutokea yaliyotokea nilikutana na Bulaya na wenzake ili dhamira yangu iniongoze, sawa wamekosea, lakini je, wapo tayari kutubu na kurudi?

“Nilichokigundua baada ya kufanya mazungumzo nao, mdomoni wanasema wanakipenda Chadema na wapo tayari kurudi na kushiriki kwenye chama, lakini tuwaachie ubunge. Binafsi nilichokigundua kinachowaweka bungeni ni masilahi ya ubunge pekee, hakuna kingine,” alisema.

Mnyika aliongeza kuwa “mwenyekiti alikuwa anafanya uamuzi kwa kusikia uchungu, lakini mimi roho yangu nyeupe kabisa… Nina amani kamili na tutawapa wabunge sahihi kabisa,” alisema Mnyika huku akipigiwa makofi.

Nini kinafuata

John Mrema alisema Baraza Kuu limekubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu ya kuwavua uanachama waliokuwa wabunge hao.

“Hatua itakayofuata Katibu Mkuu (Mnyika) ataandika barua rasmi kwa Spika wa Bunge kumtaarifu uamuzi huo. Suala hili litakuwa mikononi mwa Spika, litakuwa limetoka mikoni mwa chama.

“Kwa sasa hawana tena nafasi ya kukata rufaa, mamlaka ya rufaa yao ilikuwa mwisho Baraza Kuu, kwa hiyo hawana ngazi nyingine ya kwenda. Kwa upande wa chama tumemalizana nalo hilo,” alisema Mrema.

Kuhusu tetesi za Chadema kutaka kupeleka wabunge wengine, suala hilo halijafanyiwa uamuzi kwa sababu Kamati Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuteua wabunge.

Wabunge waliotimuliwa uanachama Chadema watinga bungeni

Advertisement