HEKAYA ZA MLEVI: Ukitaka mengineyo oa wake wawili

Sunday June 05 2022
MKE PIC
By Gaston Nunduma

Shibe mwana malevya, njaa mwana malegeza. Pale unapodhani kuwa una amani na usalama wa kutosha, tufani kuu na balaa linakuangukia usiwe na pa kukimbilia. Umejilaza kando ya bwawa la kuogelea nyuma ya kasri lako “takatifu”, unasikiliza muziki unaoupenda ukiusindikiza na kinywaji murua. Watoto na mama yao wameenda shopping mahususi kwa ajili ya kuona mambo yanakwenda sawa.

Ghafla tena bila taarifa, radi kubwa inashuka kwa kasi, inakuchapa na kukukausha kama ubua. Hakuna hodi wala taarifa; ni “PA!” na hadithi imeisha. Mambo mengine yanatisha sana. Bora basi ungepata notisi ya walau muda mfupi ungejifanya una hamu ya kazi na kukimbilia kazini. Kwa bahati mbaya unasahau kuwa utaratibu wa notisi ulishaufuta. Siku ya kiama chako usitegemee notisi.

Laiti ungelikuwa mpangaji huku uswahilini kwetu, ungelikuwa na tahadhari muda wote. Sisi tunaishi nguo zikiwa kwenye begi, simu zetu tumezitega miito ya haraka kwenda kwa bodaboda na bajaji. Likitokea la kutokea, tunaingia uvunguni na kutoka na kamba, tunabonyeza namba moja na kuongea neno moja: “Njoo!” Bodaboda inafika ungali ukimalizia kufunga godoro, kisha mwendo unatokomeza zako!

Vitabu vitakatifu vilituhadharisha tuondokane tabia ya kujiachia. Mabibi harusi walimkosa mume kwa uzembe wa kulala gizani. Bwana Mkubwa anakuja kuchukua mke, anakuta warembo wote wapo kizani kwa uzembe wa kununua mafuta. Kipo kibanda kimoja tu kinachowaka taa. Kwa jinsi alivyo fasta, anamchukua dada aliyekuwemo bila kumtazama makunyanzi wala kuuliza kama aliwahi kuwa dadapoa.

Nawezaje kusema nina amani na usalama wa kutosha? Muda unakwenda, na hakuna historia inayotuonesha kuwa ati uliwahi kurudi japo kwa nukta moja. Kama kimondo kitadondoka ni lazima kitadondoka tu. Siyo tantalila. Kawaulizeni wakazi wa Mbozi kama wao walipendelewa kiasi cha kupewa notisi wakati kimondo kinashuka.

Kwa nini basi tunakufa kwa kiu wakati mafuriko yametuzunguka? Ni kwa sababu hatukutumia mbongo zetu sawasawa. Tungekufa na kipindupindu tungeeleweka, lakini kiu? Naona hadi sasa unajiuliza “Babu Mlevi kaamka nazo au?” Hapana. Nina hasira za karibu kwa machokozi ya karibu pia. Hujaelewa bado au ujeuri?

Advertisement

Acha kwanza nikupe ramani. Unajua kwa nini majitu yenye akili sana duniani siyo mahendisamu wala mabyutifuli? Kwa sababu majitu hayo yanaangalia watu, lakini warembo hujiangalia wenyewe. Atamwangalia nani au kujifunza kwa nani wakati kila mmoja anamshangaa yeye?

Unajua kwa nini ngiri ni mkorofi na twiga ni mtulivu kupita maelezo? Ukitaka jibu la haraka jiulize ni kwa nini watu wafupi ni matata na wenye maneno mengi (aaah... siyo wote jamani). Kwa sababu yupo, ni lazima adhihirishe uwepo wake. Hii inafanana na pale unapopokea wageni wengi, ndipo mwanao mchanga anapocharuka na kuangua kilio. Bila hivyo mtajuaje kama naye yupo?

Ukitaka kujua mengineyo oa wanawake wawili (lakini usije kunihukumu, sijui huu unaoongea ni mdafu wa jana au kiroba cha leo). Mrefu aliye mrembo sana, na mfupi asiye mrembo hata kidogo (hapa nitatumia tafsida twende pamoja). Mmoja kati yao atatumia saa kumi kufanya usafi wa mwili saluni na mwingine saa kama hayo kufanya usafi wa nyumba. Ebu jijibu mwenyewe yupi atafanya lipi.

Tafiti zinatuonesha kuwa kiumbe chochote kinapohisi kuwa na mapungufu, hutafuta njia mbadala ya kuyaziba mapungufu hayo. Hali kadhalika jamii zinazojihisi kuwa haziko salama ndizo zinazojitahidi kuwasalimisha watu wake. Huwezi kuwatofautisha mama, kuku na ng’ombe kwenye ulinzi wa watoto wao katikati ya makundi ya wahuni, kunguru na mbwa mwitu.

Wakati mwingine waweza sema kujiachia ni mazoea, ambayo bila shaka yanapozidi huwa ni ulevi. Mgema anapolizoea kuti lake hadi kufikia kulipa jina, basi ujue hilo ndilo litakalomgaragaza. Mtu aliyechomwa na mwiba, akiona ujiti anashituka, lakini mtoto ambaye hajapata kuungua anaweza kuuramba moto. Kama hajakatwa na wembe basi nao ataupeleka kinywani. Bahati nzuri Watanzania wana akili na ni werevu sana. Usipotatua kero zao, watakuja kuzitatua wenyewe, shida ni njia watakazozitumia. Kwa mfano mkorofi alipoona hawezi kulipia LUKU, alicheza na mita hadi akawa akitumia bure. Kadhalika huyu aliyeshindwa kurudisha mabilioni ya benki aliyokopa kwa ujenzi wa maghorofa, alisubiri kufilisiwa na kisha akaenda kuyanunua tena maghorofa yake kwa jina la mwanaye kwa bei ya mnada.

Nchi yetu ilipata uhuru kidiplomasia. Tumechukua nchi yetu ikiwa inatapika utajiri. Sasa ninaiogopa picha ya wazazi na watoto waliokaa chakulani, mezani kuna wali, biriyani, minofu na nyama. Mtoto anagundua kuwa chakula chake kina pilipili. Anapoinua mdomo kusema “Mama, mbona...” Baba akamjibu “Wewe! Hebu kula au ntakuchapa! Kama hutaki wali si ule biriyani?”

Ni vigumu kuamini kuwa tupo kwenye amani na usalama, wakati dunia inaelewa wakulima na wafugaji wanapambana. Wanaposema “Baba, mbona wafugaji....” wanajibiwa “Ah! Kama hutaki kulima Mara si uende Rukwa?” Lazima watakuwa na woga kwenda mahali watakapoonekana wavamizi, vinginevyo wakatayarishiwe maeneo hayo kwanza.

Sera ya ardhi na makazi iwe wazi kwa kila mmoja. Kwenye hili mamlaka ziwe za kwanza kufungua milango na elimu kwa manufaa ya watu wake. Pasiwepo na kauli za “fulani dhidi ya fulani”.

Advertisement