Hekta 23 za shamba la wanyamapori zateketea Moshi
Sehemu ya shamba la wanyamapori la Namalok linalomilikiwa na kiwanda cha sukari cha TPC, wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambalo limeteketea kwa moto zaidi ya hekta 23.
Muktasari:
- Zaidi ya hekta 23 za shamba la wanyamapori la Namalok linalomilikiwa na kiwanda cha sukari cha TPC, wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro limeteketezwa kwa kwa moto na watu wasiojulikana.
Moshi. Zaidi ya hekta 23 za shamba la wanyamapori la Namalok linalomilikiwa na kiwanda cha sukari cha TPC, wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro limeteketezwa kwa kwa moto na watu wasiojulikana.
Akizungumza akiwa katika eneo hilo leo Alhamisi, Desemba 29, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ambaye aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, amesema watu waliofanya tukio hilo wanasakwa na Jeshi la Polisi.
"Nimeambiwa hili tukio sio mara ya kwanza kutokea, tukio la kwanza limetokea Mei mwaka huu ambapo hekta 21 ziliteketea kwa moto na leo hii tena hekta 23 zimeungua moto na ni tukio limejirudia mara mbili, ndani ya mwaka mmoja,
"Kwa hiyo leo tumefika hapa kuangalia hili eneo ambalo limeungua kwa moto, kuna wananchi wachache na wasiowaaminifu wanadiriki kufanya hujuma za kuchoma moto katika maeneo na kama mlivyoona hili eneo limehifadhiwa vizuri kwa ajili ya shuguli za utalii, naomba lisijirudie tena na waliofanya tukio hilo wakibainika tutawachukulia hatua,"amesema Babu
Babu amewataka wananchi wanaolizunguka eneo hilo la kiwanda kushirikiana na uongozi wa kiwanda hicho na kuacha kuchoma moto ovyo na kuharibu rasilimali zilizopo.
"Kuanzia sasa sitegemei kuona hali hii ikiendelea maana hiki kilichofanyika hapa ni jambo la kusikitisha sana maana hili eneo ni hifadhi ya wanyama iliyowekwa na ndugu zetu wa TPC na humu ndani kuna wanyama wa aina mbalimbali na wanategemewa kwa ajili ya shughuli za utalii," amesema Babu
Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, David Shilatu amesema tukio hilo limetokea Desemba 20 mwaka huu limewasababishia hasara kubwa kwasababu ni eneo hilo lina hifadhi wanyama wa aina mbalimbali kwa ajili ya shughuli za kiutalii.
"Matukio haya ya uchomaji moto yamekuwa yakijitokeza sana kwenye maeneo yetu na hili ambalo limetokea ni tukio la pili ambalo mpaka sasa ndani ya mwaka mmoja hekta 44 zimeungua kwa moto"