HESLB yaeleza sababu deni la mkopo wa elimu ya juu kuongezeka

Wednesday January 13 2021
mikopopic
By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Mwalimu Mussa Iddy wa Sekondari ya Namonge mkoani Geita, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kueleza shaka yake kuhusu deni analodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), akidai wanufaika wanaweza kustaafu nalo.

Lakini Mwananchi imepata majibu ya tatizo la deni la mkopo wa elimu kutoka HELSB, ambayo imeeleza sababu za kuonekana linakua badala ya kupungua kadri linavyolipwa.

Katika hoja zake, Mwalimu Iddy alisema hati yake ya mshahara inaonyesha deni lililobaki ambalo amekuwa akililipa kwa miaka kadhaa ni Sh4.65 milioni, lakini alipofuatilia HESLB akakuta deni ni Sh12.08 milioni.

“Ndugu watumishi na walimu wenzangu tusijipe matumaini ya kumaliza hili deni. Tunaweza hata kustaafu nalo,” aliandika Mwalimu Iddy.

Mwalimu Iddy ni mmoja kati ya zaidi ya wanafunzi 583,000 waliokopeshwa jumla ya Sh4.8 trilioni tangu mwaka 1994. Ingawa HESLB ilianzishwa mwaka 2004, imeruhusiwa kuanza kukusanya madeni ya miaka 10 nyuma.

Kati ya fedha hizo, Sh1.2 trilioni ni deni lililoiva linalopaswa kulipwa na tayari Sh872 bilioni zimerejeshwa.

Advertisement

Gazeti hili lilifanya jitihada ya kujua kikokotoo cha deni la mnufaika na mkopo wa HESLB kwa lengo la kujua mkopo huo ni vipi unageuka kuwa mzigo na namna ambavyo mnufaika anaweza kuepuka mzigo huo.

Kuhusu malalamiko ya wanufaika wa bodi hiyo akiwamo Mwalimu Iddy, mkuu wa mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole alisema ni mrejesho mzuri kutoka kwa wateja wao na wameupokea japo mengine yamepotoshwa na hayapo kama inavyosemwa.

“Mwalimu Iddy tulimtafuta tukamweleza vizuri kila kitu, malipo yote yapo kisheria,” alisema Ngole.

Sababu za deni kuongezeka

Kuhusu tatizo la deni kukua, Ngole alisema bodi ilianzisha adhabu ya asilimia 10 kwa mnufaika aliyepitisha muda wa kuanza kulipa deni lake na tozo ya asilimia sita kila mwaka, ili kulinda thamani ya fedha pamoja na gharama za usimamizi ambazo ni asilimia moja ya thamani ya mkopo.

Kwa mujibu wa mkataba wanaopewa wanufaika, adhabu ya asilimia 10 hutozwa wahitimu waliokaa zaidi ya miezi 24 bila kuanza kulipa deni.

Bila kujali kama mnufaika ameanza kulipa deni lake ndani ya muda au baadaye, ada ya asilimia sita iliyoanzishwa mwaka 2012/13 hutozwa kila mwaka katika deni ghafi ili kulinda thamani ya fedha.

Ngole alisema ili kuepuka kulipa zaidi, wanufaika wanapaswa kuanza kufanya marejesho ndani ya muda. Kwa kufanya hivyo, wataepuka faini ya asilimia 10.

Ngole alisema anayelipa mapema hupunguza kasi ya ukuaji wa deni inayotokana na asilimia sita ya kuhifadhi thamani ya fedha ambayo hutozwa kwa deni lililobaki kila mwaka.

“Tunajitahidi kuwafikia wanufaika kuwaelimisha kuwa huu ni mkopo unaopaswa kurejeshwa. Huwa tunawafuata shuleni hata katika kambi za JKT kuwapa elimu hiyo kwa kuwa wanapolipa ndipo tunapata uwezo wa kuwakopesha wengine,” alisema Ngole.

Kwa wanaojiajiri, Ngole alisema utaratibu unawataka kuanza kulipa deni lao kuanzia Sh100,000 kwa mwezi kuwaondoa kwenye orodha ya wadaiwa sugu na kuwaepusha na adhabu ya asilimia 10 kwa kupitisha muda.

Advertisement