Hifadhi ya Burigi-Chato yakabiliwa na uvamizi

Muktasari:

  • Licha ya miundombinu ya barabara na malazi katika hifadhi ya Burigi-Chato kueendelea kuboreshwa lakini inakabiliwa na uvamizi na ujangili unaofanywa na baadhi ya wakazi wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo.

Dar es Salaam. Serikali ikiwa katika juhudi za kuendelea kutafuta njia ya kuvutia watalii wengi nchini katika hifadhi ya Burigi Chato imekuwa tofauti baada ya wakazi wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo kudaiwa kuvamia na kufanya ujangili.

 Kali hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Utalii katika hifadhi hiyo, Ombeni Hingi alipopata ugeni kwa mara ya kwanza wa wacheza masumbwi kutoka mikoa ya Kagera, Mwanza na Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa pambano la kirafiki lilolenga kuhamasisha utalii lilofanyika wilayani Karagwe Septemba 24 mwaka huu.

Akizungumza kupitia Runinga ya Azam, Hingi amesema kutokana na changamoto hizo bado wanaendelea kuchukua hatua kali kudhibiti na kuhakikisha vivutio vyote vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo vinalindwa.

 “Pamoja na maboresho tunayofanya ya miundombinu kama barabara lakini changamoto kubwa ni wawindaji haramu na watu wanaoingiza mifugo kwenye hifadhi kwa ajili ya malisho,” amesema.

Hata hivyo wadau wa mchezo wa ngumi nchini, wamedai ili kutangaza vizuri vivutio vya hifadhi hiyo ni muhimu kuwatumia wacheza masumbwi zaidi kwani ushawishi wao umekuwa ukiongezeka kila siku.

“Wachezaji wa ngumi wanajulikana ndani na nje ya nchi na wamekuwa wakienda kucheza mapambano tofauti tunawatumiaje ni muhimu kuwatumia katika kutangaza vivutio vyetu,” alisema Hamis Jumanne Mkurugenzi wa HB, SADC Promotins.

Hoja iliyoungwa mkono bondia, Karim Mandonga amesema ni muhimu mapromota nchini kuchangamkia fursa hiyo kwani kutakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

Hifadhi ya Burigi-Chato ilianzishwa mwaka 2019 baada ya kupandishwa hadhi mapori ya akiba ambayo kwa sasa inapambwa na wanyama mbalimbali pamoja na Ziwa la Burigi.