Hifadhi ya jamii itakavyonufaisha wasiokuwa kwenye ajira rasmi
Muktasari:
- Uhakika huo wanaupata kupitia skimu maalumu inayotolewa na NSSF, watu hao watapata mafao kama vile pensheni ya uzeeni, bima ya afya na fidia ya ulemavu.
Dar es Salaam. Kilio cha muda mrefu cha Watanzania waliojiajiri wenyewe kukosa huduma za matibabu na kinga ya kipato baada ya nguvu kupungua, kimesikika.
Uhakika huo wanaupata kupitia skimu maalumu inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), watu hao watapata mafao kama vile pensheni ya uzeeni, bima ya afya na fidia ya ulemavu.
Skimu hiyo kwa watu wa sekta isiyo rasmi, inalenga kuwapatia ulinzi wa kijamii wale ambao hawapo kwenye ajira rasmi, kama wafanyabiashara wadogo, wakulima, wasanii hata watumishi wa ndani.
Akizungumza jana Jumanne Oktoba mosi 2024 wakati akitambulisha huduma hiyo kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omari Msiya amesema skimu hiyo inamlenga mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama katika kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa, biashara ndogo ndogo, mama lishe/baba lishe, bodaboda, machinga na wanahabari wa kujitegemea.
Amesema lengo la skimu hiyo ni kuimarisha ustawi wa jamii kwa kuweka mifumo inayowakinga dhidi ya majanga kama uzee, ulemavu, urithi, ugonjwa, gharama za matibabu, kuumia kazini, uzazi, ukosefu wa ajira na ukubwa wa familia.
Msiya amesema mtazamo na malengo ya hifadhi ya jamii katika umri wa kufanya kazi (miaka 18 hadi 60) ni kwamba kila anayejiunga anajiwekea akiba ya uzeeni, hivyo baada ya kustaafu anapata kinga dhidi ya kushuka kwa kipato.
“Hali ya maisha baada ya kustaafu itategemea na jinsi ulivyojiandaa wakati ukiwa kwenye ajira. Maandalizi endelevu na ya uhakika ni kuwa kwenye mpango wa hifadhi ya jamii,” amesema Msiya.
Mafao kwa mnufaika
Skimu hiyo inatoa mafao ya muda mfupi na ya muda mrefu ambayo ni pensheni ya uzee, urithi na mafao ya ulemavu.
Mafao ya muda mfupi ni ya uzazi, matibabu, mafao ya kujitoa (sehemu ya michango isiyozidi asilimia 50 au malipo ya mkupuo wa michango yote) na msaada wa mazishi ambayo hapo awali hayakuwahi kutolewa kwa sekta isiyo rasmi.
Akizungumzia pensheni ya uzee ambayo awali ilitolewa tu kwa waajirwa wa sekta rasmi, Msiya amesema kwa mwanachama aliyetimiza umri wa miaka 55-59 (umri wa kustaafu kwa hiari) au miaka 60 (umri wa kustaafu kisheria) na aliyechangia mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 180, atapata malipo ya mkupuo wa awali na pensheni ya kila mwezi kama wastaafu wengine.
Kuhusu pensheni ya ulemavu, alisema mwanachama anatakiwa awe amepoteza angalau theluthi mbili (2/3) ya uwezo wake wa kufanya kazi kutokana na ulemavu wa kimwili au kiakili na ulemavu huo usiwe umetokana na kazi yake.
“Mwanachama huyu anatakiwa asiwe amefikia umri wa kustaafu na awe amechangia katika mfuko si chini ya michango ya miezi 36 (miaka mitatu) na katika michango hiyo, kuwe na michango 12 iliyolipwa ndani ya kipindi alichopata ulemavu.”
Pensheni ya urithi
Akizungumzia pensheni ya urithi, Msiya amesema hiyo hulipwa kwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki ambao ni mke/mume na watoto walio na umri usiozidi miaka 18 au 21 ikiwa wanasoma.
“Iwapo warithi hao hawapo, mafao yatalipwa kwa wazazi wa mwanachama aliyefariki,” amesema na kufafanua kuwa mwanachama atakayepata pensheni hiyo, lazima awe amechangia michango isiyopungua miezi 180 (miaka 15) kabla ya kufikwa na umauti.
Alisema kwa michango chini ya miezi 180, wategemezi husika watalipwa mkupuo maalumu.
Kwa mujibu wa Msiya, mgawanyo wa pensheni ya urithi huwa kwa watoto ambao hupata asilimia 60 ya pensheni na mjane au mgane hupata asilimia 40.
Eneo jingine la mafao ni kwenye msaada wa mazishi, ambapo wategemezi wa mwanachama hulipwa kwa kiwango kati ya Sh150,000 na Sh600,000 kulingana na kiwango cha mchango wa mwezi cha marehemu.
Vigezo vya fao hilo ni kuwa mwanachama anatakiwa awe amechangia walau mara moja na awe amefariki akiwa kazini.
“Madai ya fao la mazishi yanatakiwa yafanyike ndani ya siku 60 baada ya kifo cha mwanachama,” amesema.
Tofauti na kwenye ajira rasmi, skimu hii inaruhusu fao la kujitoa, ambapo mwanachama ili aruhusiwe anatakiwa awe amechangia kuanzia miezi 12 na kwamba anaweza kutoa asilimia 50 ya michango yake au kutoa michango yake yote.
Yapo pia mafao ya uzazi, ambayo ni asilimia 100 ya wastani wa mapato ya siku ya mwanachama kwa kipindi cha miezi sita, kabla ya wiki ya 20 ya ujauzito na hulipwa kwa muda wa wiki 12, hii ni sawa na wastani wa mishahara ya miezi mitatu.
“Malipo hufanyika kwa awamu mbili, yaani 1/3 hulipwa mwezi mmoja kabla ya kujifungua na 2/3 baada ya kujifungua. Mwanachama anaweza kuamua kulipwa kwa wiki zote 12 baada ya kujifungua.
“Mwanachama awe amechangia miezi 36 (miaka mitatu) na michango 12 iwe imewasilishwa kabla ya wiki ya 36 ya ujauzito. Mafao haya yatalipwa kila baada ya miaka mitatu,” alisema.
Akiuliza maswali, Mhariri mkongwe Salim Said Salim, amehoji iwapo mwanachama atajifungua watoto pacha, mfuko unamsaidiaje?
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema mwanachama atalipa asilimia 300 ya mshahara wake au kipato chake, hivyo fao hilo linaangalia zaidi uzazi na si idadi ya watoto waliozaliwa.
Mafao ya matibabu
Kwa upande wa mafao ya matibabu, Msiya amesema hayo hutolewa kwa mwanachama na wategemezi wake ambao ni mume/mke na watoto wasiozidi wanne, wenye umri usiozidi miaka 18 na ikiwa wapo shule wasizidi miaka 21.
“Mwanachama akichangia Sh30,000 kwa mwezi atatibiwa peke yake na akichangia Sh52,200 atatibiwa yeye, mke/mume na watoto wasiozidi wanne. Mwanachama huyu anatakiwa awe amechangia angalau michango ya miezi mitatu mfululizo karibu na kupata huduma ya matibabu,” amesema.
Amesema mwanachama atapata huduma katika hospitali moja atakayochagua kutoka miongoni mwa zilizoorodheshwa na mfuko huo.
Ibrahim Yamola, mmoja wa wahariri alihoji iwapo mwanachama atapata changamoto ya kiafya akiwa nje ya mkoa aliosajili hospitali, matibabu yatakuwaje?
Akijibu hilo, Mshomba ameeleza kuna utaratibu wa kuchukua kuponi maalumu katika ofisi za NSSF ambako mwanachama amejiandikisha au atakapopata changamoto kwenye mkoa mwingine anapaswa kwenda ofisi za NSSF eneo husika na kupatiwa kuponi hizo kisha kwenda hospitali kupatiwa matibabu.
Vigezo vya kujiunga
Vigezo vya kujiunga ni lazima uwe Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 15 hadi 70, usiwe mnufaika wa mafao ya pensheni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Pia, awe na namba ya NIDA au kitambulisho chochote kinachomtambua (leseni ya udereva/mpigakura) pamoja na picha ndogo moja (passport size).