Hili ndilo jengo la Ofisi ya Benki Kuu mkoa wa Mwanza

Muktasari:

Rais Samia amezindua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Mwanza linaloelezwa kukidhi mahitaji ya benki hiyo kwa Kanda ya Ziwa.

Mwanza. Leo Juni 13, 2021 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua jengo la Ofisi ya Benki Kuu ya Tanzania tawi la Mwanza ambapo hafla hiyo imehudhuriwa na mamia ya wakazi wa mkoa huu na viongozi mbalimbali wa kitaifa, kidini na kisiasa.

 Miongoni mwa mambo ambayo wengi wanaweza kujiuliza kuhusiana na Ofisi hizo za BOT tawi la Mwanza ni pamoja na ni upi muonekano, ukubwa na matumizi ya Jengo hilo.

Akisoma risala, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Frolence Luoga amesema ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa tano umegharimu Sh42.1 bilioni likiwa ni mbadala wa jengo lililokuwa likitumika tangu mwaka 1980 kutokidhi mahitaji ya sasa kulingana na huduma za kifedha zinazotolewa na Benki Kuu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema kwamba jengo hilo lenye ghorofa tano, ghorofa zake tatu ziko chini ya ardhi ambalo linatumika kuchakata na kuhifadhia fedha.

Amesema ghorofa mbili za juu zimetumika kuanzisha eneo la mazoezi kwa ajili ya wafanyakazi, eneo la kutolea huduma za kifedha na kibenki na eneo la zahanati itakayotumika kutoa huduma ya matibabu kwa watumishi wa Benki Kuu hiyo.