Hiyo mikwara mbona benki wanakupa mkopo fasta

Hiyo mikwara mbona benki wanakupa mkopo fasta

Muktasari:

  • Hivi karibuni msanii wa muziki Bongo, Harmonize akiwa visiwani Zanzibar amedai kuwa atafanya video 100 za nyimbo zake na zitatoka mwaka huu.

Hivi karibuni msanii wa muziki Bongo, Harmonize akiwa visiwani Zanzibar amedai kuwa atafanya video 100 za nyimbo zake na zitatoka mwaka huu.

Kauli hiyo inakuja baada ya Disemba mwaka jana katika show ya Life Is Breeze ya mkali wa wimbo “Jerusalem” Master KG kutokea Afrika Kusini ambapo Harmonize alidai kila anapoonekana jukwaani akitumbuiza basi amelipwa Sh57 milioni.

Hii imekuwa ni kama tabia kwa Harmonize, kujiweka na kupanga kufanya vitu vikubwa katika muziki ingawa amekuwa akikumbana na changamoto ya kushindwa kutekeleza baadhi ya mambo kinachoweza kutafsiriwa ni kama mikwara kwa washindani wake.

Hivyo basi, makala yanakwenda kuangazia baadhi ya mambo aliyojimwambafai msanii huyo kuwa atayafanya katika muziki wake, lakini hadi sasa hayajafanyika.


1. Konde Boy mgahawa

Huu ulikuwa ni mpango wa kutoa chakula bora kwa watu ambao, hawana uwezo ambapo utaratibu wake ulikuwa ni gari la Konde Boy mgahawa kupita mtaani kila Jumapili na kugawa chakula.

Mpango huo ambao ulizinduliwa Oktoba 20, 2019 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ulitoa chakula kwa siku hiyo pekee na kuibua purukushani sana na baada ya hapo hakuna kilichoendelea.

Hata hivyo, Harmonize alikuja kueleza kuwa waliamua kuachana na utaratibu huo kwa muda kutokana na mkataba alioingia na kampuni ya kinywaji cha Sayona Twist.


2. Harmo Night Carnival

Agosti 4, mwaka jana Harmonize alitangaza tamasha kubwa “Harmo Night Carnival” litakalofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia November 28, 2020.

Harmonize alieleza kwa kushirikiana na E FM Radio na TV E Tanzania ndio watafanikisha tamasha hilo ambalo litawakutanisha wasanii wakubwa wa ndani na nje ya nchi 15.

Kubwa zaidi ilikuwa msanii atakayehitaji kutumbuiza basi alitakiwa kutoa taarifa mwenyewe na kutaja kiwango ambacho atahitaji kulipwa na muda atakaohitaji kutumbuiza.

Baada ya matangazo ya zaidi ya mwenzi mmoja kwenye vyombo hivyo vya habari, Harmo Night Carnival iliahirishwa na wahusika kueleza hadi hapo watakapotangaza tena na hadi sasa hawajafanya hivyo.


3. Ushamba Tour

Mara baada ya Harmonize kuachia wimbo wake uiitwao “Ushamba” uliombatana na uzinduzi mkubwa Dar es Salaam, alitangaza kufanya ziara (Ushamba Tour) ya kimuziki kwenye mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuutangaza na kutoa burudani kwa mashabiki wake.

Ziara hiyo ikaanza mkoani Mtwara anapotokea ambapo alifanya show na kupata mapokezi makubwa lakini baada ya hapo hakuweza kuendelea na ziara hiyo hadi sasa.

Imeandikwa na Peter Akaro