Hongera Mpango, timiza matarajio ya Watanzania

Hongera Mpango, timiza matarajio ya Watanzania

Muktasari:

  • Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Dk Phillip Mpango kuwa Makamu wa Rais juzi kisha akathibitishwa na Bunge, jana alikula kiapo ili kushika wadhifa huo kwa muda uliosalia hadi 2025.

Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Dk Phillip Mpango kuwa Makamu wa Rais juzi kisha akathibitishwa na Bunge, jana alikula kiapo ili kushika wadhifa huo kwa muda uliosalia hadi 2025.

Tunachukua fursa hii kumpongeza Dk Mpango ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Waziri wa Fedha (2016-2021), tukitambua uzoefu, uadilifu, ucha Mungu, upole na uchapaji kazi wake.

Tunasema hivyo tukitambua kuwa hata Rais Samia atakuwa anamfahamu fika Mpango kwa sababu akiwa Makamu wa Rais naye amehudumu kwa kipindi kilekile sawa na Waziri wa Fedha, hivyo kama ni kukifahamu chungu, basi anakifahamu vizuri na tunaamini ni wakati mzuri zaidi wa Dk Mpango kumsaidia Rais Samia.

Dk Mpango akiwa Waziri wa Fedha, ndiye ambaye pamoja na watendaji wengine wa Serikali, waliisaidia Serikali hadi kuingia katika uchumi wa kati.

Hatuna mashaka na uzoefu wa Dk Mpango kwa sababu pamoja na kazi nyingine, amewahi kuwa mchumi mwandamizi katika Benki ya Dunia (WB), Katibu wa Tume ya Mipango na alikuwa mshauri wa uchumi wa Jakaya Kikwete wakati huo akiwa Rais.

Kutokana na kauli yake aliyoitoa wakati akiliaga Bunge kwamba ataendelea kuwajali wanyonge na kuendeleza miradi mikubwa ya Serikali, basi Watanzania tunaweza kusema tumepata jembe, na tunaamini atamsaidia Rais kulitoa taifa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Sote tunafahamu kuwa katika kipindi akiwa Waziri wa Fedha na Mipango (2016-2020) ndicho kipindi ambacho tumeshuhudia mapato ya nchi ya yakiongezeka karibu maradufu na bajeti ikiandaliwa katika ubora wa hali ya juu.

Pamoja na sifa zote hizo na pongezi, lakini tunaamini Dk Mpango atamsaidia zaidi Rais na nchi kama atapewa fursa zaidi ya kuonyesha umahiri wake katika uchumi na kumshauri Rais kuhusu changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu.

Dk Mpango anafahamu fika kuwa, ni katika kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na taarifa nyingi za kuyumba kwa biashara na hata biashara nyingine kufungwa kutokana na kuyumba kwa sera za kodi na mifumo ya ukusanyaji.

Wala hili si la siri, kwani wafanyabiashara na wawekezaji wamekuwa wakilizungumza sana jambo hili na hata juzi tu Bungeni mara baada ya kupigiwa kura, mbunge mmoja alimuomba akamshauri Rais kuhusu suala hilo.

Wafanyabiashara na wawekezaji wana matumaini makubwa na Dk Mpango kwamba alipokuwa Waziri wa Fedha pengine kuna mambo aliyatekeleza tu kutokana na maono ya Rais, lakini sasa ni namba mbili katika uongozi.

Kwa hiyo, ni kama amebeba roho za wafanyabiashara katika suala la mfumo wa kodi kwa kuwa analifahamu si kwa kuambiwa, bali kwa kuwa sehemu ya maamuzi, hivyo ni wajibu wake sasa kumsaidia Rais kuwa na mazingira rafiki ya kodi.

Ni lazima Dk Mpango awe muumini pia wa sekta binafsi, akitambua kuwa ndiyo injini ya uchumi wowote duniani, hivyo Watanzania wanaamini atamshauri vyema Rais ili sekta hiyo irudi kama zamani katika kuchangia uchumi wa Taifa letu.

Watanzania wanaamini muunganiko wa Rais Samia, Dk Phillip Mpango, utalisaidia Taifa kufikia uchumi unaoonekana katika maisha yao ya kawaida ili wanufaike na ukuaji huo wa uchumi.