Huduma ya maji yaboreshwa kwa wanafunzi

Muktasari:

Jumla ya wanafunzi 1335 wanaosoma katika shule ya Themi jijini Arusha wataanza kufaidika na huduma ya maji, bada ya wadau kuboresha miundombinu shuleni hapo ikiwamo uchimbaji wa kisima chenye uwezo wa kutoa lita 5600.

Arusha. Jumla ya wanafunzi 1335 wanaosoma katika shule ya Themi, wamepatiwa uhakika wa maji ya kutumia baada ya kuchimbiwa kisima chenye uwezo wa kutoa zaidi ya Lita 5600 kwa saa.

Kisima hicho chenye urefu wa mita 60 kwenda chini kimechimbwa kwa ufadhili wa taasisi ya "tuelekezane peponi" yenye makao yake makuu nchini Oman.

Akizungumzia msaada huo, mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Themi, Zebedayo Mollel amesema kuwa kisima hicho kimewaokolea zaidi ya million 1.5 ambazo walikuwa wanalipia Kama bili ya maji kwa mwezi ambayo hata hivyo yalikuwa hayakidhi mahitaji ya wanafunzi.

"Tulikuwa tunatumia maji ya idara ambayo tunalipia bili kwa michango ya wazazi, lakini hata hivyo kutokana na mgawo wa Mara kwa Mara yalikuwa hayakidhi mahitaji ya wanafunzi kwa kupikia, kunywa na kuhudumia mazingira Hali iliyowapelekea wanafunzi wetu kuwa katika hatari ya magonjwa yanayotokana na uchafu"

Mollel amewashukuru wafadhili hao kutoka Oman kwa msada huo, huku akiomba Wadau wengine wajitokeze ili kuwasaidia kukarabati majengo ya madarasa yaliyochakaa na ujenzi wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi.

Nae mwanafunzi Nusrat Hussein amesema maji ya idara yaliyokuwa yanakatika mara kwa mara yalisababisha wao kushinda na kiu bila kunywa maji, lakini pia kwenda haja ndogo na kubwa bila kujisafisha huku mazingira yakiwa machafu hasa madarasa na vyoo yasiyo na hadhi kwao.

"Sisi wasichana ndio tulikuwa wahanga wakubwa zaidi kwani tulilazimika kukosa masomo kipindi cha hedhi kwa hofu ya kujisitiri kwa usafi , lakini pia  Mara kwa Mara tunaugua magonjwa ya tumbo, kuhara na hata maambukizi katika njia ya mkojo "U.T.I"

Kwa upande wake mmoja wa wafadhili kutoka "Tuelekezane peponi group", Nasr Al Jahadhamy amesema kuwa kisima hicho ni Cha 56 kuchimba nchini, vyote vikiwa na thamani ya million 560 huku wakiwa na malengo ya kusaidia zaidi panapohitajika.

"Msaada huu ni moja ya misaada mbali mbali ambayo tunatoa katika maeneo wahitaji katika nchi za Afrika, Yemen, Palestina na India, kupitia michango ya kila mwezi ya wanakundi letu la what's app la "Tuelekezane peponi" Kama kusema Asante kwa Mungu kwa kila anachotujaalia katika afya na vipato vyetu" alisema Jahadhamy


Mwenyeji wa wafadhili hao, Sheikh Ayoub  Hussein Juma, Imamu wa msikiti wa Masjid Ungalimited, amesema wafadhali hao ambao wanatoa misaada kwa jamii kupitia muongozo ya misikiti, wamefanikiwa kuchimba visima katika shule mbali mbali Arusha na kutoa misaada ya mashuka na vitanda katika shule maalumu.