Hukumu kesi ya Sabaya na wenzake leo

Aliyekua Mkuu wa wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro,Lengai Ole Sabaya (kushoto) akipunga mkono wakati akiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha pamoja na watuhumiwa wenzake kujibu tuhuma zinazowakabili jana.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Je, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya atashinda kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili au ataanza safari ya maisha jela kwa muda usiopungua miaka 30?

Arusha. Je, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya atashinda kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili au ataanza safari ya maisha jela kwa muda usiopungua miaka 30?

Majibu ya swali hili yanatarajiwa kutolewa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Odira Amworo baada ya kusikiliza kesi dhidi ya Sabaya na wenzake wawili kwa miezi miwili na nusu iliyopita.

Hatima ya Sabaya inasubiriwa kwa hamu na watu wengi kutokana na umaarufu aliojipatia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na jinsi staili yake ya uongozi iliyowagusa watu wengi kwa namna tofauti.

Tangu kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 2, kesi dhidi ya Sabaya imekuwa ikivuta watu wengi wa jiji la Arusha na maeneo ya jirani ambao wamekuwa wakijitokeza mahakamani kuisikiliza.

Kiongozi huyo ambaye mara nyingi alibainisha kama mtu wa kuogopwa, hasa na watu waliopingana na maagizo yake alikamatwa Mei 27 akiwa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha. Inadaiwa katika shtaka la kwanza kuwa Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni, Arusha, washtakiwa hao waliiba Sh2.769 milioni, mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, washtakiwa waliwashambulia Numan Jasin, Harijin Saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga kwa kutumia bunduki, ili kufanikisha wizi huo.

Katika shtaka la pili, Sabaya na wenzake wanadaiwa kuiba Sh390,000 kutoka kwa diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi wakiwa katika Mtaa wa Bondeni.

Walidaiwa kumfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku wakimtishia kwa bunduki kabla ya kufanya tukio hilo.

Sabaya na wenzake wanadaiwa katika shtaka la tatu kuiba Sh Sh35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno kutoka kwa Ramadhan Rashid wakiwa katika mtaa huohuo.

Baada ya kufanya wizi huo, walidaiwa kumfunga pingu na kumtishia Rashid kwa bastola.

Wanashtakiwa chini ya kifungu cha 287 (A) cha Kanuni ya Adhabu ambacho adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30.

Chini ya kifungu hicho, mtu yeyote anayeiba kitu chochote na kutumia silaha kutishia kabla au wakati akitekeleza wizi huo atakuwa ametenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Endapo watatiwa hatiani, Sabaya na wenzake watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela.

Washtakiwa hao wamekuwa rumande tangu kukamatwa kwao kwa sababu kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha halina dhamana kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Awali kesi ya kina Sabaya ilikuwa ikitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha lakini kuanzia Julai 18, 2021 kesi hiyo ilianza kusikilizwa mfululizo na hakimu Amworo aliyekuja Arusha akitokea Geita.