Hukumu yabatilishwa uhai umeshapotea-7

Muktasari:

  • Katika sehemu hii ya mwisho ya mfululizo wa makala hizi za ‘Hukumu ya Machozi, Damu’, miaka 70 baada ya mtoto George Stinney kuhukumiwa kifo na kunyongwa, mahakama nchini Marekani ilibaini kuwa waliosikiliza kesi hiyo, kuhukumu na kutekeleza hukumu hiyo walikosea.

Katika sehemu hii ya mwisho ya mfululizo wa makala hizi za ‘Hukumu ya Machozi, Damu’, miaka 70 baada ya mtoto George Stinney kuhukumiwa kifo na kunyongwa, mahakama nchini Marekani ilibaini kuwa waliosikiliza kesi hiyo, kuhukumu na kutekeleza hukumu hiyo walikosea.

Hivyo, George Stinney aliuawa kimakosa kwa kunyongwa kwenye kiti cha umeme Juni 16, 1944.

Stinney alitiwa hatiani kwa kuwaua wasichana wawili—Betty June (11) na Mary Emma (7), hukumu ambayo imekuwa na mwangwi kwa zaidi ya miongo saba kuanzia wakati huo.

Jumapili ya Novemba 3, 2013, ukurasa wa mbele wa gazeti la eneo la South Carolina, ‘Sumter Item’, ulikuwa na habari: “Mawakili wanataka kusikilizwa upya shauri la kijana aliyeuawa.”

Baada ya waandishi wa vitabu, habari na wacheza sinema kuitumia hukumu hiyo katika kazi zao, mwaka 2006, George Frierson, Mmarekani mweusi katika Kaunti ya Clarendon aliamua kuchunguza kwa dhati kesi hiyo. Alinukuliwa akisema “ninasadiki kwamba kijana huyu hana hatia, na siwezi kuketi tu na kuruhusu historia imrekodi kuwa ana hatia.”

Frierson hakuwa mkazi pekee wa South Carolina aliyeamua kufuatilia kesi ya Stinney. Mwaka 2009, wakili Steve McKenzie pia alikuwa ameanza kufanya utafiti juu ya hukumu hiyo. Kisha, mwaka 2013, baada ya mazungumzo kuhusu dhuluma inayofanywa na mahakama, McKenzie alihamasishwa kumshirikisha Matt Burgess utafiti wake.

McKenzie aliamini kulikuwa na dhuluma katika mahakama ambayo ilisababisha Stinney kuuawa. Burgess aliamua kuwasiliana na wanafamilia ya Stinney ambao huenda bado wako hai. Alitaka kupendekeza kesi hiyo ifunguliwe upya. Hata hivyo, dada na kaka wa George waliobaki walisitasita.

Ingawa dada mdogo wa George aliyeitwa Amie, ambaye sasa ana zaidi ya miaka 80 na ambaye siku ya tukio mwaka 1944 alikuwa na kaka yake (Stinney) wakimlisha ng’ombe wa familia, pamoja na kwamba siku zote za maisha yake alisisitiza kuwa George Stinney hakuwa na hatia, hakupendezwa sana na pendekezo la Burgess. Alimwambia Burgess “kuna Mungu anayeketi juu na anayetuona chini… tumwachie Mungu.”

Licha ya majibu hayo, Desemba 2013 Burgess alifungua kesi mpya. Alimwomba profesa wake wa zamani wa shule ya sheria, Miller Shealy amshauri. Shealy alijitolea kujiunga na timu ya wanasheria ya Stinney.

Kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa Januari 21, 2014, Jaji Carmen Mullen aliweka wazi kwamba suala hilo si kuwa George Stinney alikuwa na hatia au la, bali ni ikiwa alihukumiwa kwa haki.

Mawakili hao walipeleka mashahidi sita mbele ya Jaji Mullen. Ndugu wa Stinney—Katherine, Amie na Charles—ambao wote walikuwa wadogo mwaka wa 1944 na wakati huo (2013) walikuwa wazee kabisa.

Amie Rufner, mdogo wa ndugu wa Stinney akiwa na 78 mwaka 2014, alikuwa na umri wa miaka minane tu mwaka 1944.

Katika hati ya kiapo na katika ushuhuda wa moja kwa moja, aliapa kwamba yeye na George walikuwa wakichunga ng’ombe wa familia wakati wasichana wa Kizungu walipopita na kwamba baadaye walirudi na kubaki nyumbani pamoja kwa muda wote wa alasiri.

Baadaye alisema George aliondoka tu nyumbani wakati alifuatana na baba yake kuwatafuta wasichana waliopotea.

Kulikuwa na mambo mawili ambayo dada wa Stinney alikuwa na uhakika nayo kwamba hakuna polisi wala mawakili wa Stinney waliowahi kuwahoji kuhusu matukio ya siku hiyo na hakuna aliyeitwa kuwa shahidi katika kesi ya 1944.

Wilford Hunter, ambaye alikuwa gerezani wakati huohuo na George, katika hati yake ya kiapo, alisema Stinney alikuwa mdogo na dhaifu na akasimulia mazungumzo ambayo wawili hao walikuwa nayo walipokuwa gerezani.

Kulingana na Hunter, alipomuuliza Stinney kwa nini alikuwa gerezani, George alimjibu kwamba alishtakiwa kwa kuwaua wasichana wawili.

Timu ya McKenzie pia iliita mashahidi wawili wataalamu katika juhudi za kupinga uwezekano kwamba Stinney alikuwa amefanya mauaji hayo. Daktari wa binadamu na upelelezi, Dk Peter Stephens, aliipinga ripoti ya uchunguzi wa maiti iliyowasilishwa na Dk. Asbury Bozard kuwa haitoshi hata kwa viwango vya mwaka 1944.

Alipinga madai ya polisi kwamba George alikuwa ametumia chuma cha reli kuwaua Betty na Mary; kwamba hakuweza kubaini ni silaha gani ilitumika kuua.

Daktari wa magonjwa ya akili, Dk Amanda Salas, ambaye aliitumia kesi hiyo kuandika tasnifu yake mwaka 2010, alitoa ushuhuda wa kitaalamu juu ya kutegemewa kwa ungamo la Stinney.

Alisema bila mtu mzima kuwapo wakati wa madai ya kukiri kosa, mtoto wa miaka 14 angeshinikizwa kutoa ungamo la uongo.

Kufikia siku ya pili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, McKenzie na timu yake walitambua kuwa Jaji Mullen hangeweza kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa upya kwa sababu ushahidi wote ambao ungeweza kuthibitisha kuwa au kutokuwa na hatia—silaha ya mauaji, nguo zozote za damu, ungamo la George—ulikuwa umetoweka.

Pia, familia ya Stinney haikuwa mashahidi katika kesi hiyo kwa sababu walikatazwa kuhudhuria na hakuna mtu ambaye alikuwa katika chumba cha mahakama siku hiyo ya mwaka 1944 aliyejulikana kuwa hai mwaka 2014.

Kwa kuzingatia ubishani wa hoja za kisheria, wakili wa Stinney aliondoa ombi lake la kutaka kesi ianze upya, badala yake akaomba mahakama itazame mchakato uliotumika kusikiliza kesi ya George Stinney, kuhukumiwa na kunyongwa.

Hii iliwaruhusu kutumia ushuhuda wa mashahidi wao kwa ufanisi zaidi. Kwa nini wanafamilia ya George Stinney hawakuhojiwa? Kwa nini hawakuitwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo? Pia waliuliza maswali juu ya utetezi uliotolewa kwa Stinney mwaka 1944.

Kwa nini hakukuwa na wakili wakati George alipodaiwa kukiri kuua? Kwa nini mahakama ilishindwa kubaini ushahidi uliotofautiana kuhusu matokeo ya uchunguzi wa maiti? Kwa nini watetezi walishindwa kumhoji shahidi yeyote wa upande wa mashtaka? Kwa nini walishindwa kubadili chumba cha mahakama hata baada ya kuwapo kwa fununu za kufanyika fujo na kumuua Stinney?

Kwa nini walishindwa kukata rufaa dhidi ya hukumu ile? Timu ya McKenzie pia iliibua maswali muhimu kuhusu mchakato uliofaa katika kesi yenyewe. Kwa nini Stinney alikabiliana na mahakama iliyojaa Wazungu watupu kuanzia baraza la majaji hadi wazee wa baraza katika kaunti yenye idadi kubwa ya Wamarekani weusi?

Kwa nini kesi ya mauaji ya watu wawili ilianza alasiri na kumalizika alasiri hiyo hiyo? Pamoja na maswali haya yote kuzunguka, Miller Shealy alihisi kuwa ana haki ya kutangaza kwamba Serikali ilikuwa na “mikono michafu” kwenye kesi ya George Stinney. Kesi hiyo ilidumu kwa siku mbili, lakini ilichukua takriban mwaka mmoja kabla ya Jaji Mullen kutoa uamuzi wake. Wakati huo, kesi hiyo ilibaki hai kwenye vyombo vya habari. Ilikuwa mada ya tahariri za magazeti duniani likiwamo ‘New York Times’ na hata Jarida la ‘People’.

Desemba 17, 2014, hukumu ilitoka na ikasema: “Walikosea.” Uamuzi ulipelekwa kwa Karani wa Mahakama ya Kaunti ya Clarendon ukisema: “Mahakama hii imegundua ukiukaji wa msingi sana, wa kikatiba na wa kiutaratibu katika kesi ya 1944 dhidi ya George Stinney na hivyo inabatilisha hukumu hiyo.”

Katika uamuzi wake wa kurasa 28, Jaji Carmen Mullen alisema mahakama na upande wa mashtaka wakati huo (1944) walishindwa kulinda haki za kikatiba za George Stinney. Katika ukurasa wa mwisho wa uamuzi wake, Mullen aliukumbusha umma kwamba “ukiukaji wa haki za mshtakiwa wakati wa mchakato kesi unaharibu mashtaka dhidi yake.”

Jaji Mullen akahitimisha “haki ya kuishi ya mvulana huyo ilidhulumiwa sana na Serikali ... haki za kimsingi za mvulana zilikiukwa.”

Tangu Desemba 17, 2014, ni wazi kwamba George hakuwa na hatia. Hata hivyo, bado kuna swali moja linalotesa ambalo halijajibiwa. Ikiwa George hana hatia, basi damu ya hao waathirika watatu iko katika mikono ya nani?

Huenda jawabu halitapatikana kamwe. Lakini hukumu dhidi ya George Junius Stinney ni ya machozi na damu.