Huruma Rombo mbioni kuwa chuo kikuu cha tiba

Huruma Rombo mbioni kuwa chuo kikuu cha tiba

Muktasari:

  • Shirika la Watawa la Sisters of Our Lady of Kilimanjaro, limeanza mchakato wa kuipandisha taasisi ya tiba ya Huruma Institute of Health and Allied Sciences (HIHAS) iliyoko Rombo, mkoani Kilimanjaro, kuwa chuo kikuu cha tiba.

Moshi. Shirika la Watawa la Sisters of Our Lady of Kilimanjaro, limeanza mchakato wa kuipandisha taasisi ya tiba ya Huruma Institute of Health and Allied Sciences (HIHAS) iliyoko Rombo, mkoani Kilimanjaro, kuwa chuo kikuu cha tiba.

Hayo yameelezwa na mkuu wa shirika hilo, Sr Theresia Buretta wakati wa hafla ya uzinduzi wa chuo cha uuguzi cha Theresa kilichoko Moshi, mkoani Kilimanjaro ambapo pia kinamilikiwa na shirika hilo.

Sr Buretta amesema kumekuwepo na upungufu wa wataalamu wa afya nchini wakiwemo wauguzi na kwamba kupandishwa kwa Hihas kuwa chuo kikuu cha tiba na chuo walichoanzisha, vinaweza kuongeza chachu ya upatikanaji wa wataalamu hao.

"Mchakato wa kukipandisha chuo hicho unaendelea vyema, tayari vigezo vingi vinavyohitajika ili kufikia hatua hiyo vimefikiwa, tunaendelea na michakato na tuko mbioni kukamikisha ili kipandishwe," amesema.

Ameongeza kuwa, “Tumeboresha na bado tunaendelea kuboresha miundombinu ya pale chuoni na kitakapoanza baada ya kupewa kibali husika kitakuwa na uwezo wa kutoa shahada ya kwanza ya uuguzi.”

Akizungumzia chuo kipya cha uuguzi kilichozinduliwa, Sr Buretta amesema kuwa moja wapo ya agenda kuu ya chuo hicho ni kutoa wataalam wa afya watakaokuwa waadilifu na wenye weledi wa hali ya juu ili waweze kutoa huduma kulingana na maadili ya uuguzi yanavyoelekeza.

Amewaasa wanafunzi wa chuo hicho kipya kuhakikisha wanakuwa mfano bora wa kuigwa na wale watakaofuata chuoni hapo miaka inayokuja na kukifanya chuo hicho kuwa bora.

"Ninyi ni zao la kwanza la chuo hiki, naomba mkawe baraka, mnasoma uuguzi na kama mnavyofahamu ni kazi ambayo mtakabidhiwa uhai wa watu, naomba mkatambue nafasi zenu,"

Mkuu wa chuo hicho kipya Sr. Walter Minja, amewataka wanafunzi hao kutambua kuwa ni neema kupata fursa ya kuhudumia afya za watu jambo ambalo alisema ni muhimu kwa uhai wa mwanadamu yeyote.