Huyu Alikiba hata corona tu inamtii

Huyu Alikiba hata corona tu inamtii

Muktasari:

  • Wengi mwaka jana walinyuti. Hawakutoa kazi kwa hofu ya corona. Alikiba hakujali hilo. Katikati ya mapambano ya corona akaachia dude Dodo! Yes Dodo ilianza kama utani hivi, kadiri muda ulivyosogea watu walizidi kupagawa nayo. Noma sana.

Wengi mwaka jana walinyuti. Hawakutoa kazi kwa hofu ya corona. Alikiba hakujali hilo. Katikati ya mapambano ya corona akaachia dude Dodo! Yes Dodo ilianza kama utani hivi, kadiri muda ulivyosogea watu walizidi kupagawa nayo. Noma sana.

Kama kawaida yake ngoma zake kama moto wa pumba, huanza taratibu kama zinavyoisha taratibu. Mpaka leo hii bado Dodo linawakimbiza wasanii wengi walio toa nyimbo baada yake. Sehemu yoyote linapoamshwa Dodo utulivu hutoweka.

Leo ana “Infidele” wimbo umekamata ghafla kiasi cha wengi kushikwa na mshangao. Siku za karibuni ni kama kakasirika hivi. Kila dude la moto. Hata akishirikishwa anaua mbaya. Kamuulize Christian Bella na lile kolabo lao. Ni maumivu.

Huyu mwamba ana njia zake za pekee. Na upekee wake ndo hufanya awe mkubwa kwa wenzake wengi. Wale alioanza nao muziki na wale waliomkuta. Hata aliowakuta wengi wanamuheshimu sana. Hili usisubiri ushahidi wa kipolisi au kimahakama kujua.

Kuna wakati huwaza kivyangu kwamba siku moja akiingia studio na mwamba mwingine kama Fally Pupa itakuaje? Yes, moto utawaka. Sipati picha balaa lake, katika silaha yake ya sauti na uwezo wa kuimba. Kuna Kiba mmoja tu kwenye uso wa dunia hii ya Trump na Museven.

Kuna kitu kimoja tuwekane sawa. Muziki wa dunia nzima, kutokana na utandawazi, una maisha mafupi kuliko mbu. Pesa ya muziki kama ya soka usipowekeza ukiwa kwenye chati siku si nyingi utachekwa na hawa wanaokuzunguka kwa sasa kama mfalme.

Unapopata nafasi ya kupenya na kupiga pesa. Piga pesa kila inayokatiza mbele yako. Fanya muziki ukiwa na akili ya Mangi Mchaga wa Kibosho. Kusanya pesa zote kuliko serikali ya Magufuli. Huku ukilinda heshima yako, usiichekee pesa hata sekunde. Kamata.

Alikiba kutokana na upekee wake hili linaweza lisimuhusu sana. Kiba kadumu toka kizazi cha kina Mb Dogg mpaka hiki cha kina Rayvany. Kuna kila dalili, ingawa siyo mtabiri ila dalili za Dai kumuacha Kiba jukwaani zipo. Yes kuna tofauti.

Kiba anagonga ngoma zinazoishi. Siyo mtu wa kusubiri matukio ya kifamilia yamtengenezee wazo la wimbo.Kiba siyo mwanamuziki wa mihemko. Ndo maana ukiipiga “Seduce Me” leo na wimbo mwingine uliotoka pamoja nao utaona tofauti.

“Seduce Me” utaiona kama kitu amazing. Wakati zingine zitaonekana kama kitu cha kale mno. Nyimbo za kuvizia kitu ‘kinachotrendi’ au maneno, hazina maisha marefu. Hapa ndipo linakuja suala la wengi kuja na kumuacha Kiba palepale.

Kutokana na muziki kuwa na maisha mafupi. Kwa Marekani, baadhi ya wanamuziki hujikita kwenye filamu. 50 Cent na Ice Cube ni miongoni mwao. Wanaendelea kupiga pesa Hollywood. Muziki haudumu.

Ukiwa juu piga pesa kama vile kesho unakufa. Kusanya pesa kisha itunze mpaka ishike adabu. Usicheke na kima utachekwa wewe keshokutwa.

Unaweza kuwa siyo mtu wa klabu, mlevi wala mpenda starehe za kidunia. Lakini ukawa na udhaifu fulani ambao unateketeza pesa katika daraja lile lile la mlevi au zaidi. Kama mzinzi na mpenda anasa za kila aina.

Kama mambo ambayo mtoto wa masikini unatakiwa kuyakwepa ili kujenga baadaye yako. Na hasa kwa ajili ya watoto wako. Siri ya utajiri ni kuingiza kingi na kutumia kwa kiasi. Hakuna uchawi zaidi ya huo.

Kuna shughuli za kujionyesha kwa watu ambazo hazifanani na mtoto aliyekulia katika umasikini. Haya yatafanywa na watoto wako ambao kwa wakati huo wataitwa watoto wa matajiri. Kutokana na namna ulivyowatengenezea maisha kabla.

Huu ni wakati wa kupiga pesa, siyo kuziteketeza. Kuna wanamuziki wengine wanataka kuwa sehemu alipo staa fulani bila kupitia njia alizopita. Wanapata matajiri wawezeshaji wanaomba pesa za video ya soko la Afrika.

Wakati hata Tandale hajajulikana bado. Matokeo yake video ya milioni 50 inaenda kuingiza milioni tatu kwa shoo za Fiesta. Kutaka tu awe na video sawa na Kiba, ambaye soko lake limesambaa mpaka Sierra Leone. Unachemka.

Haraka ya matumizi makubwa ya pesa bila mipango. Pesa za kutengenezea video Afrika Kusini, tumieni kujijenga Tanzania kwanza. Pigeni pesa. Wekeza vya kutosha haya maisha unayotaka kuishi watakuja kuyaishi watoto wetu.

Akili ya kuwekeza ikajae katika vichwa vya vijamaa wote ambao kimsingi pesa zao zinaingia kupitia sanaa. Hasira za kuishi maisha duni lipiza kwa watoto wako. Sisi hata tutajirike vipi bado tutatambulika kama watoto wa masikini mpaka tunakata roho.

Na wadau wa muziki wanahitaji kubadilika kifikra. Huu siyo muda wa kukandamizana ili wapate kikubwa kuliko wavuja jasho ambao ni wasanii. Kama rahisi waambieni watoto wenu waingie studio, wafanye anachofanya Dimpoz, kisha wafanyisheni shoo za kujitolea.

Siyo kwamba Kiba hakosei, ni binadamu ana makosa mengi tu. Kaanza ‘kachenji’ kama kuchelewa kuachia madude. Pia ngoma kama Usiniseme, naamini hata yeye akiwa kivyake anakatika stimu. Siyo ngoma za daraja la Ally Saleh Kiba. Ni mapito kama mapito mengine.