Huyu ndiye Dk Tulia Ackson

Muktasari:

  • Jina la Dk Tulia Ackson lilianza kuvuma katika siasa mwaka 2014 alipoteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ila likavuma zaidi Oktoba 2015 akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Dar es Salaam. Jina la Dk Tulia Ackson lilianza kuvuma katika siasa mwaka 2014 alipoteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ila likavuma zaidi Oktoba 2015 akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Umaarufu wake wa mwaka 2015 ulitokana na kesi iliyofunguliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupinga kuzuiwa kukusanyika mita 200 kutoka kilipo kituo cha kupigia kura.

Katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, Serikali ilishinda hivyo mikutano wala mikusanyiko kutoruhusiwa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Hayati John Magufuli alimteua kuwa mbunge na akagombea unaibu Spika alioshinda kabla hajashinda ubunge wa Mbeya Mjini kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kisha kutetea nafasi yake ya Naibu Spika katika Bunge la 12.

Wadadisi wa duru za kisiasa, walitazama uteuzi huo kuwa ni sehemu ya mafanikio yaliyotokana na umahiri wake katika masuala ya sheria huku akiisaidia Serikali katika kesi zilizoikabili mahakamani.

Dk Tulia alizaliwa Novemba 23 mwaka 1976 katika Kata ya Bulyaga wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Safari yake ya elimu ilianzia Shule ya Msingi Mabonde iliyopo Tukuyu kabla hajachaguliwa kujiunga na Sekondari ya Wasichana Loleza ya Mbeya mjini na baadaye Sekondari ya Wasichana Zanaki ya jijini Dar es Salaam.

Baadaye kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosoma shahada ya kwanza ya sheria na kuhitimu mwaka 2001, na kati ya mwaka 2003 na 2007 akaenda kusoma shahada ya uzamivu Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini.

Kati ya mwaka 2001 hadi 2011, Dk Tulia alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla hajateuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.