Idris Sultan aitoa kimasomaso Tanzania Netflix

Tuesday April 27 2021
idriss pc
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Historia imeandikwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshindi wa Big Brother Africa ‘Hotshots’ mwaka 2014, Idris Sultan kuwa Mtanzania wa kwanza kuonekana katika mtandao wa Netflix.


Hatua hiyo ni kubwa kwa Idris kwa kuwa mtandao wa Netflix ni huduma namba moja duniani inayoonyesha video za filamu na tamthilia kwa njia ya kuzitazama kupitia huduma ya intaneti maarufu ‘streaming’.


Usiku wa kuamkia leo Jumanne, Aprili 27, 2021 Netflix wameanza kuionesha filamu ya ‘Slay’ ambayo mwigizaji huyo wa Kitanzania ameshiriki, ambaye ameigiza kama kijana tajiri anayetafuta mwanamke mwenye mapenzi ya kweli.

Kuonyeshwa kwa filamu hiyo ni jambo moja, lakini kupendwa kwa mwigizaji huyo duniani kwa mujibu wa maoni yaliyotolewa ni kufunguka kwa milango mingine ya mafanikio kwa Idris.


“Huwa naamka asubuhi na kuomba ila leo nimeamka na kushukuru tu. Nashukuru kwa kupata ndugu na rafiki kama ninyi.

Mshikamano, mapenzi na nguvu mliyonipa kwa miaka na kuendelea kuzidisha. Siwezi zungumza nanyi tu. Nahitaji zungumza na Mungu ili awape nisiyoweza mimi,” ameandika Idris katika ukurasa wake wa Twiter.

Advertisement


Mashabiki na watu maarufu nchini wametumia pia mtandao huo kumpongeza Idris kwa hatua hiyo aliyofikia.


Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameandika, “Nimepata wasaa wa kutazama #SlayOnNetflix na kumuona @IdrisSultan katika sinema hii. Nimefarijika sana na hatua hii aliyopiga. Ametuweka Watanzania kwenye uso wa #Netflix .

Ni mwanzo mzuri sana. Tumuunge mkono afanye vizuri zaidi na azidi kututoa kimasomaso huko mbeleni.”

Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba ameandika, “Hatimaye nimeiona Slay. Hatua kubwa kwa kijana wetu @IdrisSultan.”

Advertisement