Iguwasa kuminya zaidi upotevu wa maji

Iguwasa kuminya zaidi upotevu wa maji

Muktasari:

  • Kadri inavyouza maji mengi zaidi, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (Iguwasa) inaingiza fedha nyingi zaidi.

Tabora.  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (Iguwasa) imejipanga kupunguza kupotea kwa maji uwe chini ya asilimia 20.

Mpango huo ni sehemu ya mkakati ulioanza mwaka uliopita wa fedha ambao Iguwasa ilipunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 44 hadi asilimia 29.

Mkurugenzi Mtendaji wa Iguwasa, Hussein Nyemba amesema ili kupunguza zaidi upotevu huo, wametoa pikipiki 10 hivyo jumla kuwa 14 kwa ajili ya watumishi wake kufuatilia upotevu huo popote unapobainika.

"Vyombo hivi vitakuwa msaada mkubwa kwetu katika kufuatilia upotevu wa maji ambayo kwa mwaka mmoja uliopita tumepunguza kwa asilimia 15," amesema Nyemba.

Ili waweze kufanya shughuli zao kikamilifu na kutumia vyombo hivyo vizuri, mhandisi huyo amesema wamewapa mafunzo muhimu watumishi wote waliopewa pikipiki kwa ajili ya kufutilia upotevu wa maji.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Ally Mkalipa ameipongeza Iguwasa kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wake ili waweze kufuata sheria za usalama barabarani wanapotekekeza majukumu yao.

"Wapo baadhi ya watumishi wa Serikali wanaofikiri wapo juu ya sheria katika mambo ya usalama barabarani jambo ambao sio kweli," amesema Mkalipa.

Amewaasa watumishi  hao kufuata sheria kwa usalama wao binafsi, vyombo vyao na watumiaji wengine wa barabara.

Mmoja wa watumishi wa mamlaka hiyo, Patricia Pius ameshukuru kwa kupewa mafunzo hayo na kuahidi kuzitumia vema kufanya shughuli zao za kuhakikisha maji hayapotei pasipo sababu ili kuongeza makusanyo ya Iguwasa.

Kuanzia Disemba 2019 hadi Oktoba 2020, Nyemba anasema mamlaka hiyo ilipata Sh586.6 milioni kutoka na zaidi ya lita milioni 852.655 zilizozalishwa na kati ya Novemba 2020 hadi Septemba 2021 iliingiza Sh1.3 bilioni kutokana na lita milioni 1,500 zilizozalishwa na kuuzwa.