Ileje Sh85 milioni kuwaondoa vijana mtaani

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe  ,Farida Magomi akizungumza na wakuu wa Idara na Madiwani kwenye kikao kilichofanyika leo Mei 31,2023. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Wilaya ya Ileje inakusudia kutumia Sh85 milioni kuwaendeleza vijana waliokosa fursa za elimu ya msingi na sekondari kupitia mradi ambao umefadhiriwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (Unicef).

Mbeya. Serikali wilayani ya Ileje Mkoa wa Songwe itatumia zaidi ya Sh85 milioni kwa ajili ya vijana walishindwa kuendelea na elimu ya msingi pamoja na ile ya sekondari, kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi kupitia vituo maalum.

Mpango huo umeelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Magomi leo Mei 31, 2023 kwenye kikao cha Wakuu wa Idara na Madiwani huku akiweka bayana lengo la mradi huo kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi, hivyo kuachana na utegemezi.

“Mradi huo unatarajia kuwasaidia vijana walioshindwa kumaliza masomo au kuendelea na masomo ya msingi na sekondari kwa kupata elimu ya ufundi katika shule maalum ambayo itaanzishwa kata ya Chitete wilayani hapa,” amesema.

Amefafanua kuwa lengo ni kuwepo na mipango endelevu ya kuondoa kundi kubwa la vijana mitaani, wakiwemo waliopata mimba wakiwa na umri mdogo, ndoa za utotoni na wale waishio mazingira hatarishi, ambapo baada ya kuhitimu watawezeshwa kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowainua kiuchumi.

“Tuna kila sababu ya kutumia fursa hii vizuri, nawaomba wazazi na walezi hususan Madiwani kusemea mradi huu ili tuweze kupokea vijana wengi ambao watapata ujuzi na maarifa ya kujiajiri na hivyo kuweza kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Aidha katika hatua nyingine Magomi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ileje kuhakikisha vikundi vya vijana watakaonufaika na mradi huo vinaendelezwa na kusimamiwa na maofisa Maendeleo ya Jamii.

"Mkoa wa Songwe tumekuwa miongoni mwa halmashauri zitakazonufaika na mradi huo hususan uwepo wa vifaa kwa ajili ya kufundishia na walimu wa kutosha kulingana na idadi ya wanafunzi watakaodailiwa, hivyo, tuna kila sababu ya kuishukuru Unicef,” amesema.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hermani Njeje, amesema kuwa uwepo wa mradi huo kwa vijana waliokosa fursa ya kuendelea kielimu, ni sehemu ya suluhisho katika kuondoa kundi kubwa mitaani kwa njia ya kuwawezesha kiuchumia kupitia mafunzo hayo.

“Sasa tunakwenda kuondokana na vijana wasiofaa mitaani na hivyo kuwa na kundi kubwa lenye ujuzi na maarifa ya kujiajiri, lakini pia linaloaminika kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi endelevu ya kiuchumi,'' amesema.

Mratibu Mkuu wa Unicef nchini Dk Sempeho Siafu amesema mradi huo utakuwa na manufaa kwa vijana   kuwaunganisha na wasimamizi wa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) ili kuboresha bidhaa zitakazozalishwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya uzalishaji.