Ireland yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania

Muktasari:
- Serikali ya Ireland kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo endelevu kupitia miradi yenye tija kwa wananchi.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland, Neale Richmond, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo endelevu kupitia miradi yenye tija kwa wananchi.
Richmond ambaye anashughulikia ushirikiano wa kimataifa, maendeleo na diaspora, amesayema hayo baada ya kufanya ziara rasmi mkoani Tanga kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland.

Katika ziara hiyo iliyofanyika mwishoni mwa juma alitembelea Mradi wa Faida Maziwa, unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri), unaolenga kuboresha uzalishaji wa maziwa, kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa, na kuinua kipato cha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Aidha, ameweka mkazo katika matumizi ya mbegu bora za malisho, hatua inayosaidia kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima, na hivyo kuimarisha ustawi wa maisha ya jamii ya wakulima na wafugaji mkoani Tanga.

Pia, ametembelea kituo cha afya kinachofadhiliwa na Benjamin Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Amref, ambacho ni miongoni mwa taasisi zinazopokea msaada kutoka Serikali ya Ireland.
"Nawapongeza wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hii kwakuwa ni muhimu kuimarisha sekta za afya, kilimo, na biashara ili kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla," amesema Richmond.

Aidha katika hatua nyingine Waziri Richmond, amezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani huku wakiangazia namna ya kuendelea kushirikiana kupitia sekta za kimkakati.
Zikiwemo afya, ufugaji, uchumi wa buluu, uhifadhi wa mazingira ya pwani na baharini, uwezeshaji wa kijinsia, na maendeleo ya vijana.
Hata hivyo Dk Buriani ameishukuru Serikali ya Ireland kwa mchango wake katika miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo , hasa katika sekta za afya, ufugaji, na uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake na vijana.
"Natoa wito kwa Ireland kuangazia fursa za uwekezaji katika sekta za utafiti wa maziwa, uvuvi, na afya, pia naisisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi wa bluu kama nyenzo ya maendeleo endelevu katika mkoa huu," amesema.