Irene Uwoya, kama mvinyo wa Kitaliano

Muktasari:

  • Kesho ni Valentine Day. Wapendanao utawaona wakila bata kila kona. Yes! Ni siku ambayo rangi nyekundu huchafua mitaa yote. Inavutia siku zote. Lakini huvutia zaidi ukimiliki kiumbe bora cha kike. Kiumbe sampuli ya Irene Uwoya.

Kesho ni Valentine Day. Wapendanao utawaona wakila bata kila kona. Yes! Ni siku ambayo rangi nyekundu huchafua mitaa yote. Inavutia siku zote. Lakini huvutia zaidi ukimiliki kiumbe bora cha kike. Kiumbe sampuli ya Irene Uwoya.

Wanoko wataleta stori zao kwamba “Why Uwoya?” Unatanua taya lako hilo kindezi kuuliza hilo swali kibwegebwege. Kwamba humjui Irene Uwoya au? Yes! Ni staa. Yes! Ni mrembo haswaa. Yes! Hata mishipa yangu ya fahamu inakiri hivyo.

Miaka ya 2060, Mungu akitupa uhai tuna mengi ya kusema. Kwamba enzi hizo kulikuwa na warembo walioipamba Bongo, miongoni mwao ni Irene Uwoya. Alikimbiza kwenye umiss, filamu, ndoa na baadaye akakimbiza zaidi katika ‘usingo maza’.

Alipoweka kando umiss na kukumbatia filamu. Tukasema Uwoya ni mzuri. Siyo wa ‘sini’ wala ‘lokesheni’, bali yeye kama yeye. Baadaye wote tukasema akiigiza mahaba anajua kinoma. Kabla ya wote kukiri kuwa tuna mwigizaji wa kike mkali sana wa filamu.

Wapo walioamini kuwa ndoa ingemtoa kwenye reli. Matokeo yake akaendelea kusumbua kamera za mapaparazi kila akitua na kuondoka pale airport. Aliishi Cyprus, ajabu ni kwamba aliuza kurasa za magazeti pendwa kuliko Aunty Ezekiel aliyeishi Mwananyamala pale.

Kuna viumbe wapo duniani kwa kusudi adhimu la Mwenyezi Mungu. Kutufariji pindi tuangukapo, kutupa mizuka tutafutapo pesa, kutuzidishia hasira tunapopoteza kitu. Na zaidi kutuchangamsha akili za namna ya kutumia pesa zetu. Dunia bila kina Irene ingekuwa ngumu mno.

Kifupi ni kwamba Uwoya ni mmoja wa wasanii ambao hawaujui msamiati wa “kushuka chati”. Kila siku thamani yake inapanda juu. Kama mvinyo wa Kiyunani wenye kupikwa na Waturuki, kusindikwa kwenye chupa na Warusi, na kuhifadhiwa gharani na Wataliano. Yes!!!

Uwoya anaweza kuwa mfano tu hapa. Hakuna la zaidi katika hilo. Warembo wa aina yake huipamba tarehe 14 mwezi wa pili. Uwe mwezi wa pekee katika nyoyo zetu sisi wana wa Adam. Pita kesho maeneo ya bata. Utanielewa vizuri sana ninachokuambia.

Kila kijana wa kiume mjini anatamani kuwa na pisi kali. Na kila kijana wa mjini siku kama ya kesho ni mtihani mgumu kwake. Hapa naongelea vijana kutoka mataifa yetu ya Kusini mwa Jangwa la Sahara. Huku ndio penye shida kubwa sana kwenye hizi makitu.

Tuna tamaa kubwa ya ngono kuliko tamaa ya utajiri. Tunatamani zaidi wasichana warembo kuliko kuwapenda waungwana. Huku tunaamini Valentine Day ni maalumu kwa uzinzi. Na kwamba maana ya valentine ni kukutana kingono tu. Yes! Tunakosea sana.

Kuna mtu hana mpenzi ‘pamanenti’, lakini katumia siku mbili hizi kusaka pisi ya kutoka nayo valentine day. jiulize siku zote yeye na hiyo pisi waliishi vipi bila wenzi wao? Sisi kizazi cha mapokeo kila tuliloletewa tunaliharibu. Kama mitandao kilivyo kitu kizuri, lakini tunatumia ndivyo sivyo.

Simu zimerahisisha sana mambo. Ikiwa ni pamoja na watu kutoka ndoani kurudi kwenye usela au ‘usingo’ mama. Simu inavunja mawasiliano na watu wa karibu na kuleta walio mbali. Simu hufanya familia nyingi ziishi kibubu bubu. Na simu hupunguza umakini katika ndoa.

Waliotengeneza si lengo lao. Walitaka kurahisisha maisha katika mawasiliano kwa nia njema. Sisi tumeamua kujiongeza kama Hawa na Adam walivyojiongeza kwenye bustani ya Eden. Laana yao ndio hii inaendelea kutafuna kizazi na kizazi. Usaliti ni laana.

Umemuona Irene wa sasa? ‘Ize’, anaishi maisha yake. Humuoni na filamu wala singo ya wimbo. Lakini yupo na ni wazi kuwa maisha yake yako poa. Mwenye nafuu ya maisha huhitaji jicho la mganga kumjua. Ngozi itakueleza hata kwa picha tu ya insta.

Kuanzia pamba, ‘lokesheni’ zake ikiwa ni pamoja na ‘code’ za chimbo. Unaona kabisa hapa kuna uwekezaji wa maana usio na mawaa. Uwoya maisha yake hupanda juu miaka yote. Ubora wa Irene kwenye umiss ni tofauti na ubora wake katika Bongo Movie.

Na huyu wa leo Ni tofauti na yule wa miaka mitatu nyuma. Hafanani na shida za Bongo Movie. Wakati wengi wanalia na soko la filamu, yeye analia na wenye wivu na maisha yake. Kama comments za jealous na hasira za maisha kutoka kwa wananzengo.

Wakati wachezaji wa soka wanakuja na kuondoka wakiziacha Simba na Yanga palepale. Uwoya yeye soko la filamu limekuja na kumuacha akiwa juu kama kofia ya ‘besidei’. Hii hali hutokea kwa wachache sana. Wazungu husema ‘wani ini milioni’.

Huwezi kumuona Uwoya kwenye movie, tangazo, gazetini au hafla hizi. Lakini bado jina lake liko juu. Ukiuliza anafanya nini? Utaambiwa kila siku anabadili pozi la picha, nywele, nguo na location. Anapiga picha na kutupia insta. Baasi.

Sasa kama ni rahisi kamwambie demu wako naye afanye hivyo. Ukitaka kujua kuwa Uwoya ni nani, tangaza kwamba una ‘koneksheni’ yake. Usumbufu wake toka kwa wananzengo, utapata picha kamili ya ukubwa na mvuto wake. Kuna Uwoya mmoja tu.

Wakati wasanii wenzake alioanza nao na wale waliomtangulia kwenye sanaa yake, wakipoteza mvuto au kutoweka kwenye ramani. Kwa yeye pamoja na madhira mengi lakini jina lake na mvuto kwa mashabiki havijawahi kuyumba. Narudia tena, hatoi muvi, wimbo wala kiki... na hashuki.

Picha linaanza pisi yenyewe imesimama kinomanoma. Na picha linaisha pisi imesimama kinyama. Kuna vitu vya kujiuliza lakini. Inakuaje wasanii wengi wanaongeza idadi ya wafuasi kwenye mitandao. Lakini soko la kazi zao linatoweka? Hata tuzo za Azam jiiiii.