Jafo awaonya wawekezaji kuhusu mazingira

Friday June 11 2021
jafo pic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  Seleman Jafo amewaonya wawekezaji wanaowatumikisha washauri wa mazingira bila kuwalipa na kutumia njia za mkato kupata vyeti.

 Amesema kuna wawekezaji wanaotumia urafiki wao na wabunge au kumfahamu waziri mwenye dhamana kujaribu kupindisha kanuni na kuwaweka kando washauri elekezi wa mazingira.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 11, 2021  wakati akifungua mkutano mkuu wa tatu wa mwaka wa Chama cha Wataalam na Washauri Elekezi wa Mazingira (TEEA).

Amesema hakuna namna uwekezaji wowote unaweza kufanyika nchini bila ya tathmini ya athari ya mazingira hivyo ni muhimu kwa wataalam hao kutumika.

“Hakuna ubabaishaji kwenye kupata vyeti vya tathmini ya athari ya mazingira hata kama unafahamiana na waziri au mbunge.”

“Ni wazi kama utamfanyisha kazi mshauri halafu usimpe fedha zake huwezi kupata cheti, sasa usifikiri ukifanya hivyo unaweza kuzunguka mlango wa nyuma ukapata cheti hicho,” amesema Jaffo.

Advertisement

Amewataka wawekezaji  kutambua kuwa hakuna mbadala wa tathmini ya athari ya mazingira ni jambo wanalotakiwa kulipa kipaumbele.

Pia amewataka wataalam hao na washauri wa mazingira kuzingatia weledi kwenye utekelezaji wa jukumu hilo na kujiepusha na vitendo vya kunakili maandiko.

Mwenyekiti wa TEEA,  Profesa Hussen Sosovela amekiri kuwepo na tatizo la maadili na uadilifu kwa baadhi ya washauri  huku akiahidi kulifanyia kazi.

“Tunakemea suala hili la maadili na tunaomba baraza litusaidie na tuwaeleze wanachama wetu kuwa hatutakuwa na huruma kwa anayefanya vitendo hivi vinavyolenga kutuharibia taswira,” amesema Profesa Sosovela.


Advertisement