Jafo awaponda wanaobeza muungano

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Seleman Jafo akiangalia akimpima uzito mtoto katika kituo cha afya cha Kianga mjini Unguja kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf). Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na mazingira), Seleman Jafo amesema wanaosema muungano hauna maana yoyote wanatakiwa kupuuzwa kwa kuwa yapo mambo mengi yanayonufaisha pande zote mbili.

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na mazingira), Seleman Jafo amesema wanaosema muungano hauna maana yoyote wanatakiwa kupuuzwa kwa kuwa yapo mambo mengi yanayonufaisha pande zote mbili.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 15, 2021 alipotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Wilaya za Kaskazini na Magharibi A mjini Unguja, Zanzibar.

“Wananchi kwa ujumla tuone thamani ya muungano wetu, huu ndio unatupa mafanikio makubwa acha mambo ya mahusiano mengine, lakini katika utekelezaji wa miradi hii ambayo inagusa masuala mazima ya maendeleo.”

“Nadhani wale wanaobeza kwamba muungano hauna maana yoyote, huu ni ushahidi wa kujifunza kwamba muungano una faida kubwa sana kwa Watanzania, miongoni mwa faida na mambo mengine mengi ni haya, ujenzi wa shule na vituo vya afya,” amesema Jafo

Amesisitiza, “kwa hiyo ndugu zangu tusidanganyike na hao wanaobeza, hii ndio faida na muungano unasaidia, leo hii mtu kutoka Bara akija huku hakuna mtu wa kumuuliza yupo kwake, lakini mtu akitoka huku akaenda kuoa Bara hakuna mtu wa kumuuliza, hizi ndio faida zake.”

Amesema ni vizuri  hata wanafunzi wakafundishwa na kuelewa vyema masuala ya muungano na faida zake kuliko wale wanaopotosha ukweli.

Jafo alitembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa, kituo cha afya, soko na ukumbi wa mikutano.

Mratibu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Muungano, Khalid Bakari Hamrani amesema kupitia mfuko wa maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya tatu,  walipokea Sh12 bilioni ambazo baadhi zimetumika kutekeleza miradi hiyo.