Jaji Aboud: Mitandao ya kijamii itumike kuhimiza usawa kijinsia
Rais wa Mahakama wa Afrika ya Afrika na haki za binadamu na watu, Jaji Imani Aboud akiwa na wasichana kwenye picha ya pamoja pamoja na wadau wengine wakati alipotembelea Taasisi ya Faraja ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Muktasari:
- Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud ameitaka jamii kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yenye kuleta tija ikiwemo kuhimiza usawa wa kijinsia na kukemea vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji unaojitokeza katika jamii.
Arusha. Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud ameitaka jamii kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yenye kuleta tija ikiwemo kuhimiza usawa wa kijinsia na kukemea vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji unaojitokeza katika jamii.
Jaji Aboud ameyasema hayo leo Machi 8, 2023 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo wameadhimisha kwa kusaidia mabinti waliopata mimba za utotoni, wahanga wa ukatili, pamoja na ndoa za utotoni katika Taasisi ya Faraja Center, iliyopo kata ya Moshono jijini Arusha.
"Mitandao ya kijamii itumike kwenye mambo yanayoleta tija ikiwemo kuhimiza usawa wa jinsia katika jamii zetu na kukemea vitendo vya unyanyasaji na jinsia, unaojitokeza katika jamii zetu na kwenye mitandao ya kijamii,"amesema Jaji Imani.
Amesema mwanamke anapopewa nafasi katika jamii anaonesha umahiri katika jambo analolifanya na anaweza kuleta maendeleo na mabadiliko chanya katika nchi na jamii inayomzunguka kwa ujumla.
"Mahakama ya Afrika na Hadhi za Binadamu na Watu hapa Arusha inaungana na wenzetu ulimwenguni kusherekea Siku ya Wanawake Duniani kwa kujumika na wanawake na mabinti wa hapa Faraja, na kwa niaba ya mahakama hii natoa pongezi kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya ya kuwezesha wanawake hasa mabinti hawa wadogo kuweza kujitegemea kwa kuwapa elimu na ujuzi wa kusimamia maisha yao," amesema.
Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Faraja Center, Ester Moshi amesema kuwa mpaka sasa Taasisi hiyo imeweza kusaidia mabinti zaidi ya 500 pamoja na watoto wao na kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kueleza kuwa kituo hicho kimeleta manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
"Mwaka 2013 tulipata usajili wa kituo hiki na kimeweza kusaidia mabinti wengi waliopata mimba za utotoni zilizotokana na mazingira magumu waliyokuwa wanaishi, kwa hiyo kimekuwa ni msaada mkubwa sana kwa jamii zetu hizi zinazotuzunguka," amesema.
Hilda Yohana ambaye ni mnufaika wa Taasisi hiyo, amesema baada ya kupitia changamoto mbalimbali za maisha aliweza kusaidika katika taasisi hiyo kwa kuwa alizaa akiwa na umri mdogo.