Jaji De Mello ataka ushahidi wa kina mashauri mahakamani

Jaji De Mello ataka ushahidi wa kina mashauri mahakamani

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Jaji Joaquine De Mello amewataka wadau wote wa haki wakiwamo wapelelezi kuhakikisha kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi na zimefanyiwa utafiti wa kina ili kuwezesha utoaji haki.

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Majaji na mahakimu wanawake (TAWJA), Jaji Joaquine De Mello amewataka wadau wote wa haki wakiwamo wapelelezi kuhakikisha kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi na zimefanyiwa utafiti wa kina ili kuwezesha utoaji haki.

Jaji De Mello ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 20 wakati wa akifungua mkutano wa wadau wa haki jinai ulioandaliwa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

"Utoaji haki ni lazima ushahidi unaotolewa usiache shaka hata kidogo na Tanzania tunafuata sheria za Jumuiya ya Madola ambao kukiwa na shaka kidogo inatolewa mahakamani,” amesema.

Amewataka wadau wa mashauri wakiwamo wapelelezi kufanya utafiti na uchunguzi wa kina na kuwa na mashahidi ambao watatoa ushahidi usio na shaka ili kuwezesha utoaji haki kwa mashauri hayo.

Naye Mwanabaraka Mnyukwa wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) amesema chuo kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wadau kama majaji, mahakimu, mawakili wa Serikali na wa kujitegemea ili kushughulikia mashauri ya watoto wakiwamo wahanga wa ukatili wa kingono.