Jaji Tiganga apinga ukatili kwa watoto kumalizwa kwa usuluhishi

Muktasari:

  • Jaji Tiganga amesema pamoja na kuongezeka kwa migogoro na kulundikana kesi mahakamani, makosa ya ukatili hasa ubakaji, ulawiti, ukeketaji na mimba za utotoni hayasuluhishiki hadi mtu aliyefanya makosa hayo achukuliwe hatua stahiki.

Arusha. Jaji mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga amewatahadharisha waendesha mashitaka wa mahakama na kituo cha usuluhishi kukataa kutatua kwa njia ya suluhu makosa ya jinai hasa ya ukatili kwa watoto bila hukumu ya kisheria.

Jaji Tiganga aliyasema hayo leo Februari 1, 2023 mkoani Arusha katika kilele cha siku ya sheria nchini iliyoanza Januari 22 ikiwa na kaulimbiu 'Umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu ni wajibu wa mahakama na Wadau.'

Jaji Tiganga amesema kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu kumeongeza pia ukuaji wa uchumi na muingiliano wa biashara za kibinadamu ambazo pia zimeongeza migogoro hali inayohitaji mbinu bora za utatuzi ikiwemo usuluhishi ili kuendana na kasi ya maendeleo nchini na uchumi endelevu.

"Hata hivyo, pamoja na mbinu tunayohamasisha ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, lakini hii izingatie mashauri ya madai pekee na kamwe isihusishe jinai hasa makosa ya ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na ukeketaji.

"Nawakumbusha kuwa mashauri haya hayasuluhishiki hadi mtu yule aliyefanya makosa hayo afikishwe katika vyombo vya sheria na achukuliwe hatua stahiki ili kuendelea kudumisha amani, umoja na utengamano katika jamii," amesema.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali, Veritas Mlay amesema kuwa kutokana na idadi kubwa ya migogoro yenye asili ya madai zinazojitokeza kila siku na zile zilizoko kwenye mahakama na mabaraza ya ardhi, imekuwa changamoto kwa waendesha mashitaka walio wachache.

"Waendesha majadiliano, maridhiano na upatanishi wako 494 pekee nchi nzima idadi ambayo ni ndogo sana, hivyo ni wakati mwafaka kuboresha Sheria ya Mwenendo wa Madai sura ya 33 ili mashauri haya ya madai yasisajiliwe katika mahakama zetu bila cheti cha uthibitisho kwamba yamepitia hatua ya usuluhishi na imeshindikana," amesema.


Amesema kuwa kutatua migogoro hiyo kwa njia ya usuluhishi inawezekana na kutapunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

"Utekelezaji wa mpango huu unahitaji kuwekewa mazingira rafiki katika utekelezaji ili wahusika wote waweze kunufaika nao, hivyo tuombe wadau watoe ushirikiano mkubwa katika kufanikisha," amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema kuwa kuboresha kwa mahakama nchini imekuwa msaada mkubwa kwa Serikali hasa katika utatuzi wa migogoro hiyo ambayo pia inaleta amani na utulivu.

"Kwa umuhimu huo Serikali ya mkoa tuko tayari kutoa ushirikiano wote kwa mda wowote tutakapohitajika katika kufanikisha mashauri haya ili kuisaidia nchi kusonga mbele kiuchumi," amesema.