Jaji wa Tanzania achaguliwa tena Rais Mahakama ya Afrika
Jaji Imani Aboud, ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Arusha. Jaji Imani Aboud, ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, amechaguliwa tena kwa kipindi cha pili cha miaka miwili kuiongoza mahakama hiyo.
Jaji Imani kutoka Tanzania, amechaguliwa leo Juni 12, 2023 wakati wa ufunguzi wa kikao cha 69 cha Majaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ulioanza leo Jijini Arusha, ambapo pia Jaji Sacko Modibo kutoka nchini Mali amechaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo.
Akitoa shukrani zake, Jaji Imani aliwashukuru wafanyakazi wenzake kwa imani kubwa waliyoionyesha kwake kwa kumchagua tena kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili katika mahakama hiyo.
“Nimejawa na imani kubwa mliyonayo kwangu kwa kunichagua tena kuiongoza mahakama hii, ninawashukuruni sana," amesema Jaji Imani wakati akitoa shukrani zake.
Jaji Imani ambaye kabla ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo katika Mahakama hiyo, alikuwa ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Watu ni mahakama iliyoanzishwa na nchi za Kiafrika ili kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu na watu katika Afrika.
Mahakama hiyo ilianza shughuli zake rasmi 2006 Mjini Addis Ababa na baada ya mwaka mmoja ikahamia kwenye kiti chake cha kudumu Jijini Arusha ambapo mahakama hiyo inaundwa na majaji 11, raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.