Jamhuri watakiwa kuharakisha upelelezi mauaji ya polisi

Jamhuri watakiwa kuharakisha upelelezi mauaji ya polisi

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha kesi ya mauaji ya askari polisi katika eneo la Loliondo, wilayani Ngorongoro inayowakabili watuhumiwa 24, miongoni mwao ni madiwani 10 na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer na wananchi wengine.

Arusha. Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya askari polisi katika eneo la Loliondo, wilayani Ngorongoro, umetakiwa kuharakisha upelelezi wa shauri hilo ili watuhumiwa hao wakasikilizwe na Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

 Leo Ijumaa Agosti 5, 2022, mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilipanga kutoa uamuzi mdogo katika kesi hiyo inayowakabili watuhumiwa 24, miongoni mwao ni madiwani 10 na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer na wananchi wengine.

Hakimu Mkazi Herieth Mhenga ambaye shauri hilo la mauaji namba 11/2022 linatajwa mbele yake, aliutaka upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi wa shauri hilo.

Akitoa uamuzi mdogo kuhusu ombi la kutaka kusikilizwa shtaka la kula njama wakati shtaka la mauaji likiendelea kuchunguzwa, katika kesi hiyo, Hakimu huyo amesema mahakama hiyo haiwezi kutoa amri au kutenganisha makosa hayo na kusikiliza kosa hilo la kwanza kutokana na makosa hayo kutokea kwenye mlolongo mmoja.

Awali, Julai 14,2022 upande wa Jamhuri uliomba ahirisho kutokana na upelelezi kutokukamilika huku upande wa utetezi ukipinga na kuomba mahakama hiyo isikilize kosa hilo la kwanza la kula njama ya mauaji kutokana na mahakama hiyo kuwa na mamlaka ya kusikiliza kosa hilo.

Mawakili wa utetezi, walipinga ombi la Jamhuri la kutaka kuahirishwa kwa shauri hilo kutokana na upelelezi wa makosa hayo kutokukamilika na kueleza mahakama hiyo ya chini ina mamlaka ya kisheria kusikiliza kosa la kula njama ya mauaji.

Wakili wa Serikali, Upendo Shemkole, aliieleza Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hata washitakiwa hao waliposomewa mashitaka hawakutakiwa kujibu chochote na kuwa mashitaka hayo yametokea kwenye mlolongo mmoja hivyo hayawezi kutofautishwa.

Baada ya uamuzi wa mahakama hiyo leo, upande wa utetezi waliokuwa wakiongozwa na Wakili Ally Mhyellah, alieleza mahakama kulikuwa na kiporo cha watuhumiwa namba 18,19 na 27 ambao ni wagonjwa ambapo upande wa mashtaka walieleza watatoa uamuzi au kuleta matokeo kuhusiana na watuhumiwa hao.

Wakili wa utetezi, Maria Mushi alidai mahakamani hapo kuwa hali ya afya ya mshitakiwa wa 19, Kilooji Olojiloji, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari hali hake ni mbaya.

Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17 itakapotajwa tena.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni njama ya mauaji,ambapo kwa tarehe na sehemu isiyofahamika Ngorongoro,walipanga njama ya kuua maafisa wa serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10,2022 eneo la Ololosokwan,wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo G 4200 Koplo Garlus Mwita.