Jamii yaaswa kupiga vita ukatili
Muktasari:
Mku wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, John Tesha ameisa jamii kushiriki vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa kutoa taarifa kwa vyombo na mamlaka husika pindi vinapotokea.
Shinyanga. Mku wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, John Tesha ameisa jamii kushiriki vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa kutoa taarifa kwa vyombo na mamlaka husika pindi vinapotokea.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi na msaada wa vifaa mbalimbali kwa vikundi vya wanawake, vijana na wanafunzi mjini Shinyanga, Tesha amesema kutoa taarifa kutawezesha vyombo na mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
‘’Kupinga vitendo vya ukatili ni jukumu la kila mwanajamii popote alipo, kila mtu anao wajibu wa kutoa taarifa anaposhuhudia kitendo chochote cha ukatili na unyanyasaji kijinsia kuwezesha vyombo kuchukua hatua,’’ amesema Tesha
Amempongeza mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kuanzisha kampeni ya maswali ya chemsha bongo kupitia Radio ya Kijamii ya Faraja ya mkoani Shinyanga ambapo washindi hukabidhiwa zawadi mbalimbali.
Miongoni mwa zawadi zinazotolewa kwa washindi wa maswali ya chemsha bongo ya kupinga vitendo vya ukatili ni pamoja na majiko ya gesi, vifaa na mahitaji ya shule kwa wanafunzi na fedha taslimu.
Monica Peter, mkazi wa Mtaa wa Majengo Manispaa ya Shinyanga ambao ni kati ya waliojinyakulia zawadi ya jiko la gesi ameipongeza Serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo ofisi ya mbunge Makamba kwa kuhamasisha jamii kushiriki vita dhidi ya ukatili kupitia maswali ya chemsha bongo kwa njia ya radio.
‘’Kampeni ya kupinga ukatili kwa njia ya maswali ya chemsha bongo kwa njia ya radio imeiwezesha jamii kushiriki kikamilifu vita hivi. Tunamshukuru mbunge siyo tu kwa zawadi ya vitu, bali fedha taslim tunazozitumia kubuni na kuendesha miradi ya maendeleo,’’ amesema Monica
Mkazi wa mtaa wa Ngokolo, Getruda Felix amesema kupitia zawadi ya fedha taslim, wanawake wengi wameanzisha shughuli za kiuchumi na hivyo kuondokana na ukatili na unyanyasaji kiuchumi.
Katibu wa Chama cha Soka Manispaa ya Shinyanga, Suleiman Magubika amewahimiza vijana kuunda vikundi vya ujasiriamali kukidhi sifa ya kupata mikopo isiyo na riba kutoka halmashauri badala ya kujiweka kwenye hatari ya kujiunga kwenye vitendo vya kihalifu kwa kukaa vijiweni.
Akikabidhi zawadi kwa washindi, mbunge Makamba amewaomba wadau wengine kujitokeza kuanzisha kampeni mbalimbali kusaidia vita dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanysaji kijinsia ndani ya jamii.