Jamii yatakiwa kuzungumzia hedhi salama

Muktasari:

  • Jamii imetakiwa kutoona aibu kuzungumzia suala hilo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya hedhi salama inayoadhimishwa Mei 28.

Dar es Salaam. Wakati siku ya kimataifa ya hedhi ikitarajiwa kuadhimishwa Mei 28, jamii imetakiwa kuvunja ukimya kuhusu elimu ya hedhi salama na kuanza kuwafundisha watoto wa kike tangu wakiwa shule za msingi.

Elimu hiyo itawasaidia watoto kutambua mabadiliko ya mwili yanapotokea na kujitunza dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayosumbua wanawake kwa sasa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa taasisi ya  Somo na Mwari, Asnat Masoud wakati akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Ali Hassan Mwinyi kuhusu elimu ya hedhi salama sambamba na kugawa taulo za kike kwa wasichana shuleni hapo.

Amesema utamaduni wa kufanya hedhi suala la siri unawagharimu watoto wengi wa kike kwa kuwa wanakosa elimu sahihi jambo linalohatarisha afya zao.

“Tusione aibu kuzungumza kuhusu hedhi, wazazi wakizungumza na watoto wao na kuwafundisha namna ya kujiweka safi wakati wa hedhi itapunguza haya maradhi ambayo yameshika kasi kwa wanawake.

“Utasikia kuna fangasi, saratani ya shingo ya kizazi magonjwa haya yanatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutojiweka safi wakati wa hedhi, kuna wasichana wanakaa na taulo moja kwa siku nzima.

Pamoja na usafi wakati wa hedhi, Asnat anasisitiza jamii kuwapa elimu ya kujitambua watoto wa kike ili kuwanusuru na vishawishi ambavyo wanaweza kukutana navyo baada ya kuvunja ungo.


Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Esta Manjuna amesema kwa hali ilivyo sasa ni muhimu wazazi na walimu wakashirikiana katika kutoa elimu ya hedhi na afya ya uzazi kwa wanafunzi kuwajengea uwezo wa kujitambua.

“Tumefurahi wadau hawa wamekuja kutoa elimu kwa wanafunzi wetu wa kike, naamini itawasaidia kwa kiasi fulani maana siku hizi wazazi hawana muda wa kuzungumza na watoto.

“Elimu ya hedhi salama inapaswa kuingizwa kwa watoto wa kike wayatambue mabadiliko yao ya kimwili na namna ya kujitunza wasijiingize katika mazingira hatarishi,” amesema