Jela miaka 30 kwa kubaka mwanafunzi

Jela miaka 30 kwa kubaka mwanafunzi

Muktasari:

  • Ryoba Ngobiro (25) mkazi wa kijiji cha Kitunguruma kata ya Mbalibali amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili  shule ya sekondari Kitunguruma.

Serengeti. Ryoba Ngobiro (25) mkazi wa kijiji cha Kitunguruma kata ya Mbalibali amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili  shule ya sekondari Kitunguruma.

Hukumu hiyo katika kesi ya jinai namba 103/2019 imetolewa leo Jumanne Aprili 13, 2021 na hakimu mkazi wa Wilaya ya Serengeti, Adelina Mzalifu  baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kutorosha mwanafunzi, kubaka na kumpa mimba mwanafunzi kinyume cha sheria.

Amesema katika kosa la kwanza la kutorosha mwanafunzi adhabu yake ni miezi sita jela na kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela  na kwamba milango ya rufaa iko wazi.

Awali mwendesha mashtaka wa Serikali,   Paskael Nkenyenge amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 23,2019 na Desemba 4,2019 alifikishwa mahakamani.

Amebainisha kuwa mahakama haina rekodi ya makosa ya mshtakiwa lakini ameomba mahakama kutoa adhabu kulingana na sheria kwa makosa aliyoshitakiwa nayo huku mshtakiwa huyo akiomba kupunguziwa adhabu.