Jela miaka 30 kwa kukutwa na nyama ya pofu, swala

Jela miaka 30 kwa kukutwa na nyama ya pofu, swala

Muktasari:

  • Mkazi wa kijiji cha Emboreet wilayani Simanjiro, Gerald Kashiro amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Manyara kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuhifadhi nyara za Serikali.

Babati. Mkazi wa kijiji cha Emboreet wilayani Simanjiro, Gerald Kashiro  amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Manyara kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuhifadhi nyara za Serikali.

Hakimu wa Mahakama ya mkoa wa Manyara, Juma Mwambago ametoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi namba 21/2019  jana Alhamisi Mei 13, 2021  mjini Babati baada ya Kashiro kutiwa hatiani na ushahidi usiokuwa na mashaka.

Awali, mwendesha mashtaka, Rusticus Mahundi amesema Kashiro alipatikana na nyara za Serikali Oktoba 8, 2019 katika kijiji cha Emboreet wilaya ya Simanjiro.

Mahundi amesema  nyara hizo za Serikali ni nyama ya pofu yenye thamani ya Dola 1,700  za Marekani sawa na Sh3.9 milioni.

Amebainisha kuwa pia alikamatwa na nyama ya swala ya Sh4.9 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Amesema kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 86 (1) (2) (c) cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba tano ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 59 (a) (b) cha mabadiliko ya sheria ya mwaka 2016.

Amesema ikisomeka na aya ya 14 ya kwanza na kifungu 57(1) na 60(2) cha sheria ya kuhujumu uchumi sura ya 200 ya mwaka 2002 pamoja na mabadiliko ya kifungu cha 16(a) na 13(b) kwa pamoja ya sheria namba 3 ya mwaka 2016.