Jela miaka 31 kumpa mimba mwanafunzi

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga, imemhukumu kwenda jela miaka 31 mkazi wa mji wa Handeni Wilaya humo, Ibrahim Mgaza kwa makosa matatu, likiwamo la kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi.


Kilindi. Mahakama ya Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga, imemhukumu kwenda jela miaka 31 mkazi wa mji wa Handeni Wilaya humo, Ibrahim Mgaza kwa makosa matatu, likiwamo la kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, John Chacha alisema licha ya utetezi wa mshtakiwa, mahakama hiyo imemtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka 31.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Chacha alisema mshitakiwa alitenda kosa la kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1), (2) (e) na 131(1) cha sheria ya adhabu ya makosa ya jinai sura ya 16 R.E 2019 na kosa la pili, ni la kumpa ujauzito mwanafunzi kinyume cha kifunga 60.A (3) cha sheria ya elimu kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria na 2/2016.

Hakimu huyo alisema kosa la tatu, ni la kumtorosha mwanafunzi kutoka kwa wazazi wake kinyume na kifungu cha 134 na 35 cha sheria ya adhabu ya makosa ya jinai sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Awali, mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Seif Makono alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa la kubaka kati ya Julai na Septemba 28, 2021 na kosa la kumtorosha alilitekeleza kati ya Agosti 2, 2021 na 24, 2021.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo akiwa katika Kijiji cha Mafisa kilichopo Kata ya Mvungwe Wilaya ya Kilindi kwa kumrubuni mtoto huyo na kumtoroshea Handeni, huku akijua kuwa ni mwanafunzi na ni kosa kisheria.

Hivyo, mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo na wale wanaofikiria kutenda makosa kama hayo.

Akiomba mbele ya hakimu kabla ya kupewa adhabu, mshtakiwa aliiomba mahakama imuonee huruma kwa sababu ni mara yake ya kwanza kutenda kosa kama hilo na anategemewa na familia hivyo kuwa jela familia yake itaathirika.