JICHO LETU MAHAKAMANI: ‘Damu iliyochukuliwa Pande ilikuwa ya binadamu’ (53)

JICHO LETU MAHAKAMANI: ‘Damu iliyochukuliwa Pande ilikuwa ya binadamu’ (53)

Muktasari:

  • Katika sehemu ya 52 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, shahidi wa 36, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Sidney Mkumbi, pamoja na mambo mengine alieleza mshtakiwa wa 11, Koplo Rashid Lema alivyowapeleka eneo la mauaji msituni na kuchukua sampuli za damu iliyokuwa imeganda kwenye udongo.

Katika sehemu ya 52 ya simulizi hii ya Kesi ya Zombe, shahidi wa 36, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Sidney Mkumbi, pamoja na mambo mengine alieleza mshtakiwa wa 11, Koplo Rashid Lema alivyowapeleka eneo la mauaji msituni na kuchukua sampuli za damu iliyokuwa imeganda kwenye udongo.

Hii ni simulizi ya Kesi ya Zombe, kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na askari polisi wengine 11.

Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini watatu kutoka Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo, mdogo wake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, dereva teksi wa Manzese Dar es Salaama, aliyekuwa akiwaendesha.

Walikuwa wakidaiwa kuwapiga risasi katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2006, baada ya kuwatia mbaroni Sinza Palestina, nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, walipokuwa wamempelekea mkewe pesa, wakihusishwa na uporaji wa pesa katika gari la kampuni ya Bidco.

Katika sehemu ya 53 tutaangazia ushahidi wa shahidi wa 37. Huyu alikuwa ni nani, alihusikaje katika kesi hii na ni nini alichokisema: Endelea kufuatilia sehemu hii…

Shahidi wa 37 na wa mwisho kwa upande wa mashtaka alikuwa ni Mkemia Mkuu wa Serikali Daraja la II kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias.

Katika ushahidi wake, Septemba 25, 2008, akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Angaza Mwipopo, aliieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa sampuli za damu zilizokuwa zimegandamana na udongo zilizochukuliwa kutoka msituni Pande, mahali wachimba madini wale walipouliwa.

Kwa mujibu wa maelezo ya ushahidi wake mahakamani hapo, Machi 9, 2006, akiwa ofisini alipokea vielelezo kutoka kwa Inspekta Omari Amir Omari (shahidi wa 31) katika kesi hiyo, kutoka makao makuu ya upelelezi.

Vielelezo hivyo vilikuwa ni sampuli nne za udongo uliodaiwa kuwa na damu pamoja na barua ya maombi ya kufanya uchunguzi wa sampuli hizo.

Barua hiyo ilikuwa ikimtaka achunguze na kuchangua iwapo udongo huo ulikuwa na damu na kubainisha kama ilikuwa ni damu ya binadamu au ni ya wanyama na pia kubainisha makundi ya damu hizo kama ni za binadamu.

Kwa kuzingatia maelekezo ya barua hiyo ya maombi ya kufanya uchunguzi, alifanya uchunguzi wa sampuli hizo kisha akaandaa taarifa ya matokeo ya uchunguzi, ambayo aliikabidhi kwa aliyekuwa amepeleka barua ya maombi ya uchunguzi huo.

Ripoti hiyo ya uchunguzi wa sampuli hizo iliwasilishwa na kupokewa mahakama kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Akiizungumzia ripoti hiyo, shahidi hiyo aliieleza mahakama kuwa kwanza alichanganya sampuli hizo na kemikali maalumu yenye uwezo wa kutambua kama katika udongo huo kulikuwa na damu, na kwamba matokeo yake yalionesha kuwa ilikuwa ni damu.

Katika hatua ya pili alieleza kuwa alichanganya kemikali nyingine kwa ajili ya kubaini damu hiyo ni ya binadamu au ya mnyama na matokeo yake akabaini kuwa ilikuwa n damu ya binadamu,

Hata hivyo alieleza kuwa hakuweza kubaini kundi la damu kwa kuwa chembe chembe zinazoweza kugundua kundi la damu zilikuwa zimeshaharibika.

Katika uchunguzi wake alibaini kuwa damu iliyokuwemo katika udongo huo ilikuwa ni ya binadamu.

Hata hivyo alieleza kuwa kutokana na kuoza kwa seli za damu hakuweza kubaini makundi ya damu hizo.

Mara baada ya kutoa ushahidi, mawakili wa upande wa utetezi pamoja na washauri wa mahakama walimuuliza shahidi huyo maswali mbalimbali kuhusiana na uchunguzi wake na sehemu ya mahojiano kati yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Gaudioz Ishengoma: Lile furushi (sampuli ya udongo uliokuwa na damu) lilikuwa ni kulinganisha?

Shahidi: Lengo lilikuwa kujua kama ni damu na si kuwa na ulinganifu.

Wakili: Ni katika mazingira yapi huweza kusababisha chembechembe za damu zinaweza kuharibika?

Shahidi: Mazingira kama vile unyevunyevu, mvua na joto

Wakili Majura Magafu: Shahidi, ulipokea maombi ya uchunguzi sampuli nne za udongo kutoka kituo gani cha polisi?

Shahidi: Kutoka kwa OC-CID, Oysterbay.

Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa kitambulisho cha damu huwa ni chembechembe na si rangi?

Shahidi: Ndio, kuna chembechembe zinazounda damu lakini mimi ninazungumzia zinazoweza kutambulisha kundi la damu.

Jaji Salum Massati: Umelielewa swali lake? Alihoji jaji na kumtaka wakili Magafu arudie swali ili shahidi asikie vizuri na Magafu aliporudia swali hilo shahidi alijibu “Ndio”.

Wakili: Kwa hiyo hizo seli ndizo zinazoweza kutambulisha kuwa hii ni damu na hii siyo damu?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ni muda gani ambao seli zinaweza kuchukua hadi zisiweze kutambulisha kuwa hii ni damu?

Shahidi: Hutegemea hali ya mahali pale ilipo damu hiyo kama mvua haijanyesha.

Wakili: Ndio maana ninauliza kama mvua inanyesha au inapigwa na jua na wadudu wanapitapita, je, inachukua muda gani hadi seli kuharibika? Ni wiki nane, na ni siku 2 au ni muda gani?

Shahidi:Kama mvua inanyesha si rahisi kuweza kutambua aina ya kundi.

Jaji: Mbona unakimbilia kundi? Anauliza ni muda gani hadi damu iharibike?

Shahidi: Inategemea muda na hali inayoizunguka damu hiyo mahali ilipo.

Wakili: Sasa katika mazingira hayo itachukua muda gani, mwezi wiki mbili siku tatu. Je, inachukua muda gani hadi isiweze kutambulika?

Shahidi: Mazingira niliyotaja yakitokea inaweza kuharibika.

Jaji: Labda nikuulize swali, damu ile ilikuwa na muda gani?

Shahidi: Siyo rahisi kutambua ni muda gani. Sisi hutumia kemikali ambayo inakwenda hadi kwenye damu. Kemikali hizo nikizichanganya zinatoa matokeo.

Wakili: Kwanini Mkemia Mkuu wa Serikali huthibitisha (ripoti ya uchunguzi wa sampuli) huwa anakuwepo au huamini tu (kuwa ni sahihi).

Shahidi: Ripoti lazima ihakikiwe na mkuu wangu, hivyo ili naye awe anaelewa kila kitu.

Wakili: Hivyo yeye anatizama tu ulichokiandika wewe au naye anarudi pale? (maabara).

Shahidi: Lazima ajiridhishe ndipo tunasaini.

Wakili: Anarudi maabara?

Shahidi:Ananiuliza ninamwelezea na kumwonyesha

Wakili: Kwa hiyo mnarudia tena?

Shahidi: Lazima ajiridhishe na athibitishe maana inahusu maisha ya watu.

Wakili Rongino Myovela: Shahidi, ni wakati gani hiyo kemikali ya Anti-sera inashindwa kutoa matokeo sahihi?

Shahidi: Kwanza inategemea na uhifadhi wake, ni lazima iwe imehifadhiwa katika hali inayostahili kwa mfano katika friji, lakini kama ikitolewa nje haiwezi kufaa tena.

Wakili: Nani anatunza friji ya kuhifadhia kemikali hiyo?

Shahidi: Inatunzwa katika ofisi ya mkemia mkuu.

Wakili: Wewe una friji hiyo ofisini kwako?

Shahidi: Sina.

Wakili: Nikisema kwa sababu wewe siyo mtunza friji ya kemikali hiyo bali ni mtu mwingine kwa hiyo huna uhakika kama zilitunzwa sahihi na kwamba kwa hali hiyo hata yale matokeo hayakuwa sahihi utasemaje?

Shahidi: Si kweli.

Wakili: Kwa nini?

Shahidi: Lazima kabla ya kuanza uchunguzi tunatest ant-sera kama inafanya kazi, kama ikikataa huna haja kuendelea nayo tena.

Wakili: Katika utambuzi wenu wa damu kama ni ya binadamu au ni ya mnyama kuna asilimia ngapi za kutokea makosa?

Shahidi: Zile kemikali makosa yake huwa ni kidogo sana mara nyingi usahihi wake ni asilimia 99.9.

Wakili: Wewe ulipata wapi hizo takwimu?

Shahidi: Kutokana na kumbukumbu za ubora wa chunguzi tunazofanya.

Wakili: Nikisema hiyo asilimia 0.1 inayosalia ndio ilisababisha matokeo yasiyo sahihi katika uchunguzi wako unaoutolea ushahidi huu unasemaje?

Shahidi: Usahihi niliousema ndio huohuo.

Wakili: Kwakuwa kwa utaalamu wako na shule yako huwezi kueleza zaidi ya hapo, (alisema wakili Myovela huku akikaa).

Wakili Denis Msafiri: Shahidi, umesema ulibaini kuwa ile ilikuwa ni damu, lakini udongo una mchanganyiko wa vitu vingi, je, una uhakika gani kama ile kemikali haikuweza kuharibiwa na udongo hivyo ikashindwa kutoa matokeo sahihi?

Shahidi: Kabla ya kufanya uchunguzi tunaifanyia majaribio ile kemikali kisha tunatenganisha ile damu na udongo.

Wakili: Umesema ulishindwa kubaini makundi ya damu, je, naweza kuwa sahihi nikisema ile sampuli ya udongo uliyoletewa ilikuwa ni moja lakini ikagawanywa katika sehemu nne?

Shahidi: Sababu nilizozitoa ni kwamba chembechembe za damu zilikuwa zimeharibika. Kama ilikuwa ni moja au ngapi mimi sijui,

Wakili: Unafahamu mchanganuo wa udongo?

Shahidi: Nafahamu.

Wakili: Je, uliweza kuchunguza kama udongo ule ulikuwa ni wa aina moja au aina tofautitofauti?

Shahidi: Maombi ya uchunguzi niliyoletewa yalikuwa kutambua kama katika udongo huo kuna damu na kama damu hiyo ni ya binadamu au ya mnyama na kisha kutambua makundi ya damu hiyo. Hivyo mimi nilibaki kwenye maswali niliyotakiwa kuyatolea majibu tu, alijibu shahidi huyo huku washauri wa mahakama wakitikisa vichwa.


Inaendelea kesho